'
Sunday, January 27, 2013
KOCHA SIMBA ALALAMIKIA KIWANGO
LICHA ya Simba kuanza vyema mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mfaransa, Patrick Leiwig, amesema hajaridhishwa na kiwango cha timu yake.
Simba ilianza mzunguko huo juzi kwa kuifunga African Lyon mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya pambano hilo, Leiwig alisema licha ya Simba kushinda mchezo huo, kiwango hakikuwa cha kuridhisha.
Kocha huyo alisema anataka kuona kiwango cha Simba kikiwa juu zaidi katika mechi zijazo kwa timu kucheza kwa kujituma zaidi.
Leiwig, ambaye juzi ilikuwa mara yake ya kwanza kuishuhudia Simba ikicheza katika ligi, pia alieleza kutoridhishwa na hali ya hewa ya Dar es Salaam hivi sasa, ambayo alilalamika kuwa joto ni kali mno.
Alisema baridi iliyokuwepo Oman, ambako timu hiyo ilikwenda kuweka kambi ya wiki mbili, imewaathiri wachezaji wake, ambao sasa wanacheza mashindano katika mji wenye joto.
Kocha huyo alisema hali ya hewa ya Oman ilikuwa digrii 22 na kuongeza kuwa, itachukua muda kidogo kwa wachezaji kuzoea kucheza katika mazingira ya joto.
Leiwig aliwataka mashabiki wa Simba wasivunjike nguvu kutokana na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake juzi, badala yake wajiandae kuona soka ya kiwango cha juu katika mechi zijazo.
Simba inatarajiwa kushuka tena dimbani Februari 3 mwaka huu kumenyana na JKT Ruvu mjini Dar es Salaam kabla ya kumenyana na JKT Oljoro katika mechi itakayopigwa Februari 9 mjini Arusha.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment