KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 15, 2013

SIWEZI KUACHA MUZIKI WA INJILI-STARA

MWANAMUZIKI anayechipukia katika muziki wa Injili nchini, Stara Thomas amesema kamwe hawezi kuachana na muziki huo kwa sababu ni kazi ya kumtumikia Mungu.

Stara alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, uamuzi wake wa kupiga tena muziki wa kizazi kipya, hauna maana kwamba ameamua kuachana na muziki wa Injili.

Mwanamuziki huyo, ambaye mwaka jana aliamua kuokoka na kupiga muziki wa Injili, alisema kupiga muziki wa kizazi kipya kwake ni kazi ya ziada kwa ajili ya kujiongezea kipato.

"Nitafanya muziki wa kizazi kipya kama kazi, lakini siwezi kuacha muziki wa Injili," alisema mwanamuziki huyo, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa wakati alipokuwa akipiga muziki wa miondoko ya zouk na rhumba.

"Nitaendelea kumtumikia Mungu. Nitakapomaliza kupiga muziki wa kizazi kipya, narudi kumtumikia Mungu. Nikipata pesa, naweza kuwasaidia wajane na kufanyakazi zingine za kijamii na za kanisa,"aliongeza mwanamama huyo mwenye watoto wawili.

Stara alisema kwake, kazi ni kazi, cha msingi ni kufuata na kuheshimu maadili ya dini na kumtumikia Mungu. Mwanamuziki huyo mkongwe aliachia albamu yake ya kwanza ya Injili mwaka jana, inayojulikana kwa jina la 'Nani mshamba', ikiwa na vibao vinane.

Mbali na kibao cha Nani alaumiwe, vibao vingine vilivyomo kwenye albamu hiyo ni Petro, Safari ya Wanaisrael, Niambie, Yesu alipokuja, Hauna jibu, Soma Biblia na Jesus You are the hero.

Stara alisema albamu hiyo ni mwanzo wa safari yake ndefu ya kupiga muziki wa Injili na amewataka wapenzi wa muziki huo kujiweka sawa kupokea nyimbo zake nyingine, ikiwa ni pamoja na kuanzisha bendi yake ya muziki huo.

Kabla ya kuamua kuyaweka maisha yake mikononi mwa Yesu, Stara alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na vibao vyake maridhawa kama vile Sikia, Sitorudi nyuma, My body, Children rights na Nipigia, alioshirikishwa na msanii AT.

Awali, Stara alikuwa muumini wa dhehebu la Jamatrine, lakini kwa sasa ni muumini wa kanisa la Shalom lililoko Mbezi Salasala, Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment