TIMU ya soka ya Yanga jana iliichapa Black Leopards ya Afrika Kusini mabao 3-2 katika mechi ya kirafiki ya kimataifa ya soka iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Yanga tangu iliporejea nchini kutoka Uturuki, ambako ilikwenda kuweka kambi ya wiki mbili kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Iliwachukua Yanga dakika 30 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa kwa njia ya penalti na Jerry Tegete baada ya Haruna Niyonzima kuangushwa ndani ya eneo la hatari. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Black Leopards ilisawazishadakika ya 46 kwa bao lililofungwa na Humphrey Khoza baada ya kuunganisha wavuni kwa kichwa, kona iliyopigwa na Rodney Ramagalela.
Frank Domayo aliiongezea Yanga bao la pili dakika ya 70 kabla ya Tegete kuongeza la tatu kwa mkwaju mkali, uliotinga moja kwa moja wavuni.
Zikiwa zimesalia dakika mbili pambano hilo kumalizika, Leopards iliongeza bao la pili kupitia kwa Muganga Diunga kwa njia ya penalti baada ya Juma Abdul kumchezea vibaya Edgar ndani ya eneo la hatari.
No comments:
Post a Comment