LONDON, England BEKI wa kati wa kimataifa wa Zambia, Stopilla Sunzu yuko nchini England ambako anafanyiwa majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya Reading.
Sunzu (23) kwa sasa anaichezea klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na anatarajiwa kuichezea Zambia katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zinazotarajiwa kuanza Jumamosi nchini Afrika Kusini.
Beki huyo wa kimataifa wa Zambia, anatarajiwa kutumia wiki moja kufanyiwa majaribio na Reading kabla ya kurejea kwenye kikosi cha Zambia.
Mabingwa watetezi Zambia wamepangwa kuanza michuano hiyo kwa kumenyana na Ethiopia. Taarifa iliyotolewa na tovuti ya Reading juzi ilisema kuwa, Sunzu alipewa ruhusa na Chama cha Soka cha Zambia pamoja na TP Mazembe ya kuondoka kwa muda kwenye kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo ili kufanya mazoezi na Reading na kupimwa uwezo na makocha wa timu hiyo.
"Stoppila atajiunga tena kwenye kikosi cha Zambia baadaye wiki hii, kabla ya kucheza mechi yao ya kwanza ya fainali za Mataifa ya Afrika Jumatatu ijayo," ilieleza taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, licha ya kuichezea TP Mazembe ya DRC, Sunzu anafahamika vyema na Kocha Mkuu wa Reading, Brian McDermott kutokana na kuwepo kwenye kikosi cha vijana cha timu hiyo alipokuwa mdogo.
Reading ilisema kupitia taarifa hiyo kuwa, Sunzu atafanyiwa majaribio kwa siku nne ili makocha waweze kuona uwezo wake kabla ya kuamua kumsajili kwenye dirisha dogo.
Sunzu ni miongoni mwa wachezaji walioteuliwa kuwania tuzo ya mwanasoka bora wa Afrika mwaka jana.
Beki huyo ndiye aliyeifungia Zambia penalti ya mwisho katika mechi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana na kuibuka na ushindi wa penalti 8-7 dhidi ya Ivory Coast.
Mbali na Sunzu, tayari Reading imeshamsajili beki Stephen Kelly kutoka Fulham, kiungo Hope Akpan kutoka Crawley na Daniel Carrico kutoka Sporting Lisbon ya Ureno wakati wa dirisha dogo.
No comments:
Post a Comment