TUSKER ya Kenya juzi ilifuzu kucheza fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Mapinduzi baada ya kuichapa Miembeni ya Zanzibar mabao 2-0 katika mechi ya nusu fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Kwa ushindi huo, Tusker sasa itakutana na Azam katika mechi ya fainali itakayopigwa leo kwenye uwanja huo. Azam ilifuzu kucheza fainali baada ya kuichapa Simba kwa penalti 5-4.
Pamoja na timu zote mbili kucheza kwa kushambulia katika kipindi cha kwanza kwa lengo la kupata mabao, hadi mapumziko hakuna iliyoweza kupata bao.
Tusker ilibadili staili ya mchezo katika kipindi cha pili na kufanikiwa kufunga mabao mawili dakika ya 52 na 72 kupitia kwa Luke Ochieng na Jesse Were.
Wakati huo huo, Kocha Msaidizi wa Azam, Kalimagonga Ongara ametamba kuwa, wana kila sababu ya kuifunga Tusker leo na kutwaa Kombe la Mapinduzi.
Ongara alisema mjini hapa juzi kuwa, japokuwa Tusker ni timu iliyokamilika katika kila idara, vijana wake wana ari kubwa ya kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo.
Hata hivyo, Ongara alikiri kuwa pambano hilo litakuwa gumu kwa sababu wapinzani wao ni timu nzuri na wanacheza kwa ushirikiano mkubwa.
“Itakuwa mechi ngumu kwa sababu Tusker ni wazuri, lakini hata sisi timu yetu ni nzuri, hivyo tutapigana kiume kuhakikisha tunashinda na kutwaa ubingwa,"alisema.
No comments:
Post a Comment