JOHANNESBURG, Afrika Kusini
ANGOLA na Morocco juzi zilishindwa kutambiana baada ya kutoka suluhu katika mechi ya kundi A ya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa kwenye uwanja wa FNB mjini hapa.
Katika mechi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali, timu zote mbili zilipata nafasi kadhaa za kufunga mabao, lakini zilishindwa kuzitumia vyema.
Mshambuliaji, Younes Belhanda, aliyeingia kipindi cha pili, nusura aifungie bao Morocco katika kipindi cha pili baada ya kuitoka ngome ya Angola, lakini shuti lake lilitoka sentimita chache pembeni ya goli.
Angola nayo ingeweza kupata bao katika kipindi hicho wakati mshambuliaji wake, Guilherme Afonso alipoingia na mpira ndani ya eneo la hatari na kubaki na kipa Nadir Lamyaghri wa Morocco, lakini shuti lake lilitoka nje.
Kocha Rachid Taoussi wa Morocco aliamua kumweka benchi Belhanda katika kipindi cha kwanza kutokana na kuwa na wasiwasi na afya yake, lakini alilazimika kumuingiza kipindi cha pili kwa lengo la kuongeza kasi ya mashambulizi.
Angola ilikuwa ya kwanza kufanya mashambulizi kwenye lango la Morocco kipindi cha kwanza wakati Mingo Bille alipofumua kiki kali iliyopanguliwa na kipa Lamyaghri.
Morocco ilijibu mashambulizi wakati Abdelaziz Barranda na Oussama Assaidi walipokuwa wakiichachafya mara kwa mara ngome ya wapinzani wao na kusababisha mpira uchezwe ndani ya eneo la Angola.
Akizungumza baada ya pambano hilo, Kocha Rachid wa Morocco alisema walistahili kushinda mechi hiyo kutokana na kupata nafasi nyingi za kufunga mabao, lakini walishindwa kuzitumia.
Kocha Mkuu wa Angola,Gustavo Ferrin alisema sare hiyo imewapa faraja kubwa kwa vile timu yake haikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.
No comments:
Post a Comment