CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kimeandaa mdahalo kwa ajili ya wagombea wa nafasi za juu za uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mdahalo huo umepangwa kufanyika Februari 15 mwaka huu.
Mhando alisema uamuzi wa kuendesha mdahalo huo ulifikiwa wakati wa kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika jana, ambapo pamoja na mambo mengine, kilijadili masuala mbalimbali.
"Kikao kimeiagiza sekreterieti ya TASWA ifanye maandalizi ya mdahalo huo kwa kuzungumza na vituo vya televisheni ili uweze kuonyeshwa moja kwa moja kwenye vituo hivyo ili wananchi waweze kuwasikiliza wagombea,"alisema.
Mhando alisema mazungumzo ya awali na wadhamini mbalimbali yameanza kwa ajili ya kufanikisha tukio hilo la kuendesha mdahalo huo laivu kwenye televisheni. Alisema nafasi ambazo wahusika watafanyiwa mdahalo ni ya rais na makamu wa rais.
TASWA ilianza kufanya midahalo kwa wagombea wa nafasi za juu katika uchaguzi wa TFF kuanzia 2001 na 2004. Mdahalo wa kwanza kuonyeshwa laivu ulikuwa wa 2008.
Kwa mujibu wa Mhando, chama chake kitawasiliana na uongozi wa juu wa TFF ili kiweze kutoa msaada wa kufanikisha mdahalo huo.
"Tunaamini ushirikiano uliopo kati ya TFF na TASWA utasaidia kwa namna fulani kufanikisha jambo hilo na mdahalo huo utahusisha waandishi wa habari waandamizi wa michezo, wahariri wa baadhi ya vyombo vya habari vya michezo na wadau wachache wa soka,"alisema.
Mhando alisema tayari Kamati ya Utendaji ya TASWA imemteua mwandishi wa habari mkongwe, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio ABM, Abdallah Majura kuwa mwendeshaji wa mdahalo huo kutokana na uzoefu wake katika masuala ya habari na mambo ya michezo.
Katibu Mkuu huyo alisema chama chake hakiungi mkono mgombea yeyote na haina mpango wa kumuunga mkono mgombea yeyote.
"TASWA inaonya kuwa, kama kuna baadhi ya wagombea wenye ndoto za kutaka kutumia mgongo wa TASWA ili wapate mteremko kufikia malengo yao, hazitatimia,"alisema Mhando.
Amewataka waandishi wa habari za michezo nchini kuzidisha umakini katika kipindi hiki cha uchaguzi wa TFF na kujiepusha na makundi ya aina yoyote, ambayo yatatia doa taaluma ya habari.
No comments:
Post a Comment