KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 27, 2013

MUUMIN, SONYO, GEORGE GAMA WAIBUKIA VICTORIA SOUND



NA RASHID MUSSA, MTWARA

UNAPOWAZUNGUMZIA wanamuziki wenye tabia ya kuhamahama kutoka bendi moja hadi nyingine hapa nchini, bila shaka jina la Muumin Mwinjuma haliwezi kukosekana. Kama ni orodha ya wanamuziki 10 wanaoongoza kwa tabia hiyo, jina la Mwinjuma lazima liwemo.

Ni mwanamuziki aliyepitia bendi nyingi hapa nchini na hata katika nchi jirani ya Kenya. Aliwahi kupiga muziki katika bendi za Mchinga Sound, Double M Sound na Bwagamoyo Sound, ambazo alikuwa akiziongoza na Twanga Pepeta International.

Na sasa ameanzisha bendi nyingine mpya inayojulikana kwa jina la Victoria Sound, ambayo imeweka kambi mkoani Mtwara, ikiandaa nyimbo mpya. Lengo la Muumin ni kuifanya bendi hiyo itishe.

Katika maisha yake kimuziki, Muumin amewahi kutunga nyimbo nyingi zilizompatia sifa na umaarufu mkubwa. Lakini vibao vya Mgumba namba moja na namba mbili na Kilio cha Yatima ndivyo alivyoviimba akiwa Double M Sound ndivyo vitakavyobaki kwenye kumbukumbu ya mashabiki wa muziki kwa muda mrefu ujao.

Sifa kubwa ya Muumin katika muziki ni sauti yake maridhawa. Wapo baadhi ya waimbaji wenye sifa na uwezo wa kuiga sauti za wanamuziki mbalimbali maarufu, lakini kuiga sauti ya Muumin kunahitaji sifa ya ziada.

Ndio sababu siku alipoondoka Mchinga Sound, wanamuziki wa bendi hiyo pamoja na mmiliki wake waliona wazi kuwa, ulikuwa mwisho wao. Walipatwa na hisia hiyo kwa sababu Muumin aliimba karibu nyimbo zote za bendi hiyo na hakukuwa na mwenye uwezo wa kuiga sauti yake.

Je, ni kwa nini Muumin ameamua kujiengua katika bendi ya Twanga Pepeta International na kuanzisha bendi mpya ya Victoria Sound? Je, bendi hii itaweza kudumu kwa muda mrefu? Mbona aliwahi kuanzisha Bwagamoyo Sound lakini ikafa?

Maswali hayo na mengineyo kadhaa ndiyo yaliyonishawishi nimtafute Muumin baada ya kupata taarifa kwamba yupo Mtwara, akiwa amejichimbia na bendi yake hiyo ya Victoria Sound.

Akizungumza na Uhuru mwishoni mwa wiki iliyopita mjini hapa, Muumin alisema kuhama kutoka bendi moja hadi nyingine ni jambo, ambalo haliwezi kuzuilika kwa mwanamuziki, lengo likiwa ni kutafuta malisho mazuri.

Muumin alisema inawezekana wapo baadhi ya wanamuziki wanaohama bendi kwa malengo mengine, lakini kwake siku zote amekuwa akitafuta malisho mazuri na pia kuinua vipaji vya wengine.

Hata hivyo, mwimbaji huyo mkongwe hakutaka kuzungumzia kiundani kuhusu suala hilo la kuhamahama kutoka bendi moja hadi nyingine kwa madai kuwa, majibu aliyoyatoa yanatosha.

Lakini alitamba kuwa, ana hakika bendi hiyo itadumu kwa muda mrefu kutokana na kujiimarisha katika kila idara na pia kuundwa na wanamuziki wengi wenye vipaji vya muziki.

Alisema uamuzi wao wa kuweka kambi Mtwara ulilenga kuwapa muda wa kutosha wa kutunga nyimbo mpya na kuzifanyia mazoezi kabla ya kuanza rasmi maonyesho yao kwenye kumbi mbalimbali za burudani.

Muumin alisema bendi ya Victoria Sound sio mpya kwa sababu ilianzishwa miaka sita iliyopita. Alisema kilichofanyika ni kuisuka upya.

"Tumekuja hapa Mtwara tangu mwishoni mwa mwaka jana na lengo letu kubwa la kuweka kambi hapa ni kutafuta utulivu, utakaotuwezesha kufanyakazi yetu kwa umakini mkubwa,"alisema mwimbaji huyo.

Alisema kambi yao imekuwa na mafanikio makubwa kutokana na kupata ushirikiano mzuri na huduma nzuri kutoka kwa wenyeji wao. Alisema tangu walipoanza kambi, wamekuwa wakifanya mazoezi saa nane kwa siku.

Muumin alisema tayari wameshatunga vibao vipya vinne na walianza kuwaonjesha uhondo wake wakazi wa Mtwara mwishoni mwa wiki iliyopita katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya Bandari.

Alivitaja vibao hivyo vipya kuwa ni Shamba la Bibi na Utafiti wa mapenzi, alivyovitunga yeye mwenyewe. Aliviita vibao hivyo kuwa ni moto wa kuotea mbali.

Vibao vingine ni Mama Bahati, kilichotungwa na mpiga gita la rythm, Yohana Mbatizaji na Mwisho wa siku, kilichotungwa na Waziri Sonyo.

"Kwa watakaovisikia vibao hivyo kwa mara ya kwanza, wataelewa ni kwa nini tuliamua kuja kuweka kambi Bagamoyo kwa sababu si vya mchezo,"alisema Muumin.

Baada ya onyesho hilo la Mtwara, bendi hiyo ilitarajia kuwapa burudani wakazi wa mkoa wa Lindi kabla ya kurejea Dar es Salaam. Makao makuu ya bendi hiyo yapo Mbagala-Kiburugwa.

Kwa mujibu wa Muumin, mara baada ya bendi hiyo kurejea Dar es Salaam, itakwenda moja kwa moja studio kwa ajili ya kurekodi nyimbo hizo nne. Alisema wanataka kurekodi albamu, itakayokuwa na nyimbo saba.

Muumin amewataka mashabiki wa muziki nchini kujiandaa kupata burudani ya aina yake kutoka katika bendi hiyo, ambayo alijigamba kuwa, wapinzani wao wakubwa watakuwa Twanga Pepeta na FM Academia.

Mbali na Muumin, Sonyo na Yohana, wanamuziki wengine wanaounda bendi hiyo ni Selemani Mumba, anayepiga gita la solo na Moshi Hamisi, anayepiga kinanda.

Wengine ni George Gama, anayepiga magita yote matatu, Januari Joseph, Ciana Jordan, Ramso Bushoke, Jonas Mlembuka na Mussa Kalenga, ambao ni waimbaji.

Wanamuziki wengine wanaounda bendi hiyo ni Kassim Mumba, anayepiga gita la besi, Abdalla Hussein anayepiga kinanda na Vaninga Swalehe,anayepiga tumba.

Bendi hiyo inakamilishwa na wacheza shoo, Omari Mussa 'Bokilo', Joha Juma, Mariam Othaman, Farida Omari, Lilian Wayanga, Nadia Benjamin na Sophia Ramadhani.

No comments:

Post a Comment