KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 22, 2013

NAPATA TABU KUCHAGUA MWANAMKE WA KUOA-UKWA

LAGOS, Nigeria

MCHEZA filamu machachari wa Nigeria, Osita Iheme, maarufu zaidi kwa jina la Ukwa amesema anapata tabu kuchagua mwanamke wa kufunga naye ndoa.

Akihojiwa na mtandao wa Express Entertainment wiki iliyopita, Ukwa alisema ana marafiki wengi wa kike, lakini kila linapokuja suala la kuchagua mke, anashikwa na kigugumizi.

"Tatizo ni kwamba sielewi nani anayenifaa kumuoa. Ninao marafiki wengi wa kike na mashabiki, lakini nashindwa," alisema mcheza filamu huyo mwenye umbo fupi.

"Kumchagua mtu, ambaye nitaishi naye maisha yangu yote ndicho kinachonichelewesha kufunga ndoa. Mungu atanisaidia kuamua hivi karibuni kwa sababu kwake, kila kitu kinawezekana,"aliongeza.

Ukwa alianza kupata umaarufu mwaka 2002 baada ya kushirikiana na Chinedu Ikedieze 'Aki' kucheza filamu ya Aki na Ukwa na tangu wakati huo, wamekuwa marafiki wakubwa.

Hata hivyo, Aki aliamua kuachana na maisha ya ukapera mwaka juzi baada ya kufunga ndoa, hali inayomfanya Ukwa ajihisi kuwa mpweke.

Mapema mwaka jana, Ukwa alisema bado hajajua ni lini atafunga ndoa na atamuoa nani.

Ukwa alielezea msimamo wake huo, kufuatia ndugu, jamaa na marafiki kumuhoji mara kwa mara wakitaka kujua ni lini atafunga ndoa.

Ukwa alikiri kuwa, anajisikia vibaya kuona kuwa, swahiba wake huyo amefunga ndoa huku yeye akiwa bado anamsaka mchumba wa kumuoa.

"Sielewi lini nitafunga ndoa, lakini naelewa kwamba wakati utakapofika, kila mmoja atafahamu. Siwezi kueleza ni lini nitafanya hivyo," alisema Ukwa.

"Mungu ananitayarishia njia kwa ajili yangu nami naelekea katika njia hiyo. Nitakapofika, kila mmoja atafahamu."

"Siwezi kusema kama tayari ninaye mchumba ninayetarajia kufunga naye ndoa. Wapo wanawake wengi sehemu mbali mbali duniani. Ni jukumu langu kumsikiliza Mungu atakapozungumza nami na kunionyesha mwanamke sahihi. Wakati utakapofika, nitachagua mwanamke huyo,"alisema Ukwa.

No comments:

Post a Comment