KUNDI la pili la wachezaji tisa wa klabu ya Simba linatarajiwa kuondoka nchini leo kwenda Oman kwa ajili ya kambi ya wiki mbili.
Wachezaji hao wanaondoka leo baada ya wengine wanane kuondoka nchini juzi kwenda Oman kwa ajili ya kambi hiyo ya mazoezi.
Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kiwhelo 'Julio' alisema jana kuwa, kundi hilo la pili la wachezaji linatarajiwa kuondoka saa 10:00 jioni kwa ndege ya Shirika la Emirates.
Julio alisema wameamua kuondoka leo badala ya Jumapili baada ya timu hiyo kutolewa mapema katika michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa kufungwa kwa penalti 5-4 na Azam.
Aliwataja wachezaji watakaoondoka leo kuwa ni William Mweta, Miraj Adam, Paul Ngalema, Hassan Isihaka, Komabil Keita, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Abdallah Seseme na Said Demla.
Julio alisema anaamini kuwa, kambi ya Oman itazidi kuiimarisha timu yake ili iweze kufanya vizuri katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara na mashindano ya klabu bingwa Afrika.
Kocha huyo alisema ushiriki wao katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi umewasaidia kujenga kikosi imara na pia kuwapa uzoefu zaidi wachezaji waliopandishwa kutoka kikosi cha pili.
"Tumepata mazoezi mazuri katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi na sasa tunaelekeza nguvu katika kambi ya Oman ili tuweze kujiimarisha na kuongeza viwango vya wachezaji wetu," alisema Julio.
Mshindi kati ya Simba na Azam ilibidi apatikane kwa njia ya penalti tano tano baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya bao 2-2. Katika mechi hiyo, Simba ilitumia wachezaji wa kikosi chake cha pili.
No comments:
Post a Comment