KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 22, 2013

SENDEU, MWESIGWA WAMJIA JUU MANJI

SIKU moja baada ya uongozi wa klabu ya Yanga kutangaza kuwafuta uanachama, aliyekuwa katibu mkuu, Celestine Mwesigwa na ofisa habari, Louis Sendeu, viongozi hao wa zamani wamesema uongozi umekurupuka.

Wakizungumza na Uhuru kwa nyakati tofauti mjini Dar es Salaam jana, Mwesigwa na Sendeu walisema, uongozi wa Yanga ulikurupuka kuwasilisha ajenda hiyo kwa wanachama bila kufuata katiba ya klabu hiyo.

Mwesigwa na Sendeu walifukuzwa kazi Agosti mwaka jana kwa madai ya kushindwa kutekeleza vyema majukumu yao kabla ya kufutwa uanachama juzi kwa kosa la kuishitaki klabu hiyo mahakamani.

Akifafanua, Mwesigwa alisema haiwezekani kwa uongozi kumfuta uanachama mwanachama wake kwa sababu ya kudai haki yake ya msingi.

Alisema haki ya mtu na mapenzi kwa klabu ni vitu viwili tofauti na kwamba walikuwa na kila sababu ya kudai haki yao mahakamani baada ya uongozi kushindwa kuwalipa madai yao.

Mwesigwa alisema kwa hali ilivyo, klabu ya Yanga kwa sasa inaelekea pabaya kutokana na mtu mmoja kuamua kila jambo bila kuomba ushauri wa viongozi wenzake.

"Ndani ya miezi minne ya uongozi mpya, wanachama watatu tumefutwa uanachama! Je, ukifika mwaka mmoja hali itakuwaje? Hii itakuwa klabu au mali ya mtu binafsi?" Alihoji Mwesigwa.

Alisema anachotambua ni kwamba bado yeye ni mwanachama halali wa Yanga na kwamba maamuzi yaliyotolewa na wanachama katika mkutano wa juzi yalilenga kumfurahisha mtu mmoja.

"Klabu ya Yanga kwa sasa ipo mikononi mwa mtu mmoja, ambaye akiamka asubuhi, anakuwa na uwezo wa kuamua lolote analotaka hata kama halina maslahi kwa wanachama," alisema Mwesigwa.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa Yanga alisema, ataendelea kudai haki yake mahakamni hadi uongozi utakapoamua kumlipa madai yake kwa vile haki ya mtu haiwezi kupotea bure.

Kwa upande wake, Sendeu alisema kitendo cha uongozi wa Yanga kuwasilisha ajenda ya kuwajadili mbele ya wanachama ni sawa na kuidharau mahakamani kwa vile suala hilo tayari lipo mahakamani.

Sendeu alisema pia kuwa, uongozi wa Yanga ulifanya makosa kuwahukumu kabla ya kuwaita kwa ajili ya kuwahoji na kusikiliza utetezi wao.

Msemaji huyo wa zamani wa Yanga alisema pia kuwa, mkutano wa wanachama ulioitishwa juzi ni batili kwa vile wanachama hawakupewa ajenda siku 21 kabla ya mkutano kama katiba inavyoelekeza, badala yake walipewa ndani ya ukumbi wa mkutano.

"Hii maana yake ni kwamba, wanachama hawakupata muda wa kuijadili ajenda hiyo na zinginezo kwa muda unaotakiwa ili waweze kuijadili na kibaya zaidi, uongozi uliingia mkutanoni ukiwa tayari na maamuzi,"alisema Sendeu.

Alidai kuwa upo uwezekano mkubwa kwa mkutano huo kuhudhuriwa na wanachama hai na wasiokuwa hai kutokana na utaratibu mbovu uliotumika kuuitisha na kutolipwa kwa ada za uanachama.

Alisisitiza kuwa, vyovyote itakavyokuwa, lazima uongozi wa Yanga umlipe madai yake kwa vile ni halali na kwamba hatakuwa tayari kuona haki yake ikidhulumiwa.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Manji alisema Mwesigwa na Sendeu wamefutwa uanachama kwa kosa la kuishitaki klabu hiyo mahakamani. Mwesigwa ameishitaki klabu hiyo kwa kuidai sh. 183,400,050 wakati Sendeu anaidai sh. 79,900.050.

No comments:

Post a Comment