KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts amesema, kukaa pamoja na wachezaji kwa muda wa wiki mbili wakati timu ilipokuwa kambini nhini Uturuki, kumemwezesha kupata muda wa kujenga kikosi imara.
Brandts alisema wakati alipoanza kuinoa timu hiyo mwishoni mwa mwaka jana, aliikuta ikishiriki kwenye mashindano ya ligi, hivyo hakupata muda wa kuijenga timu.
"Lakini kambi ya Uturuki imeniwezesha kufanikisha hilo kwa vile nimekaa na wachezaji kwa muda mrefu, kujua uwezo wao na kuwajenga kisoka,"alisema kocha huyo alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam jana.
Kocha huyo kutoka Uholanzi alisema pia kuwa, kambi ya Uturuki imesaidia kuongeza kiwango cha wachezaji na kuwafanya wacheze kwa ushirikiano zaidi.
Alisema ana hakika mazoezi ya Uturuki yataiwezesha timu yake kufanya vizuri katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Hata hivyo, Brandts alikiri kuwa, bado timu yake inahitaji mazoezi zaidi kwa lengo la kujiimarisha.
Yanga iliweka kambi katika mji wa Antalya nchini Uturuki ikiwa ni pamoja na kucheza mechi tatu za kirafiki kwa ajili ya kujiandaa na hatua ya pili ya ligi kuu.
Wakati huo huo, Kampuni ya Prime Time Promotions imesema maandalizi ya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Yanga na Black Leopards ya Afrika Kusini yanakwenda vizuri.
Mwakilishi wa kampuni hiyo, Shaffih Dauda aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Black Leopards inatarajiwa kutua nchini kesho ikiwa na kikosi cha watu 37 wakiwemo wachezaji na viongozi.
"Tuanatarajia mchezo kati ya Yanga na Black Leopards utakuwa mzuri na Yanga itaweza kujipima vyema kwani itacheza na timu ambayo ipo katika kiwango kizuri," alisema Dauda.
Dauda alisema kutokana na Yanga kuwa kambini kwa wiki mbili nchini Uturuki, anaamini mashabiki watapata burudani safi kutoka kwa mabingwa hao wa Kombe la Kagame.
Alivitaja viingilio katika mchezo huo kuwa ni sh. 30,000 kwa VIP A, sh. 20,000 kwa VIP B na sh. 15,000 kwa VIP C. Jukwaa la rangi ya chungwa kiingilio kitakuwa sh. 7,000/ wakati jukwa la rangi ya bluu na kijani mzunguko ni sh. 5,000.
No comments:
Post a Comment