KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Kim Poulsen, ameondoka nchini jana kwenda Afrika Kusini kuzifuatilia timu za Ivory Coast na Morocco.
Ivory Coast na Morocco ni miongoni mwa timu zinazoshiriki katika fainali za mwaka huu za Kombe la Mataifa ya Afrika na zimepangwa kundi moja na Taifa Stars katika fainali za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia za 2014.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, Poulsen amepanga kutazama mechi za timu hizo ili kupima uwezo wake kabla ya kukabiliana na Taifa Stars.
Wambura alisema baada ya kutazama mechi hizo, kocha huyo kutoka Denmark atapata nafasi ya kupanga mbinu za kukabiliana nazo.
Alisema hiyo ni miongoni mwa mikakati iliyoandaliwa na TFF ili kuhakikisha Taifa Stars inafanya vizuri katika michuano hiyo na kufuzu kucheza fainali zitakazochezwa nchini Brazil.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, inashika nafasi ya pili katika kundi lake. Itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment