KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 22, 2013

LULU AOMBA DHAMANA MAHAKAMA KUU, MAOMBI YAKE KUSIKILIZWA IJUMAA

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imepokea maombi ya dhamana ya msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael 'Lulu' na imepanga kuyasikiliza Ijumaa wiki hii.

 Taarifa zilizopatikana mahakamani hapo wiki iliyopita zimeeleza kuwa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Zainabu Mruke.

Lulu, ambaye anasota rumande katika gereza la Segerea, anakabiliwa na mashitaka ya kumuua bila kukusudia, aliyekuwa msanii mwenzake, Steven Kanumba kinyume cha kifungu cha 195 cha Kanuni za Adhabu.

Awali msanii huyo alikuwa akikabiliwa na shitaka la kuuwa kwa kukusudia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini baada ya upelelezi kukamilika, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), alimbadilishia mashitaka na kuwa ya kuua bila kukusudia.

Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, ulimsomea mshitakiwa huyo maelezo ya mashahidi Desemba 21, mwaka 2012. Baada ya kusomewa maelezo hayo, kesi hiyo ilihamishiwa Mahakama Kuu, ambayo ndiyo yenye uwezo wa kusikiliza mashitaka yanayomkabili.

Shauri hilo la kuua bila kukusudia tayari limesajiliwa na kupewa namba 125/2012 katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.

Lulu kwa kupitia jopo la mawakili wanaomtetea, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Masawe, amewasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa kosa linalomkabili linaweza kumfanya apate dhamana.

Mawakili hao wamewasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura, wakiomba yasikilizwe na kuamriwa mapema kwa kuwa Lulu amekaa rumande kwa miezi saba na kosa lake linadhaminika.

Kwa mujibu wa hati ya maombi, iliyoambatanishwa na hati ya kiapo, Wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba Mahakama iamuru mshitakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo itaona yanafaa.

"Tunaiomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshitakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, lililopo katika mahakama hii tukufu,” ilisema sehemu ya hati ya maombi.

Wakili Kibatala pia ameeleza kupitia hati hiyo kwamba, muombaji anao wadhamini wa kuaminika, ambao wako tayari kufika mahakamani kama wadhamini kwa niaba yake.

Katika hati hiyo, Wakili Kibatala pia amedai kuwa, iwapo mshitakiwa atakubaliwa dhamana, yuko tayari na ataweza kutimiza masharti yote ya dhamana yatakayotolewa na mahakama.

Wakili Kibatala amedai kuwa kwa muda ambao ameiendesha kesi hiyo, amepata fursa kubwa ya kufahamiana na muombaji pamoja na familia yake na kwamba kwa msingi huo, anajua kuwa muombaji huyo ana tabia nzuri na ni wa kuaminika.

Wakili huyo pia ameeleza kupitia kwenye hati hiyo kwamba, muombaji bado yuko chini ya uangalizi wa wazazi wake, ambao wako tayari kuhakikisha anatimiza masharti na anafika mahakamani wakati wowote kadri atakavyohitajika kwa ajili ya usikilizwaji wa shauri lake au kusudi lolote.

“Muombaji ni mtu maarufu na mkazi wa Dar es Salaam, hivyo kwa mazingira haya ni rahisi kumfuatilia katika utekelezaji wa masharti yoyote ya dhamana. Kama wakili wake (Kibatala) niko tayari, kutimiza wajibu wangu kuhakikisha muombaji anatimia masharti yote kikamilifu na kufika mahakamani kadri na wakati atakapohitajika," alidai Wakili huyo.

Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, April 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican, Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Shadrack Kimaro, umedai kuwa utaita mashahidi tisa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.

Kimaro pia aliieleza mahakama kuwa, atawasilisha vielezo kadhaa vitakavyotumika kama sehemu ya ushahidi katika kesi hiyo, ikiwemo ramani ya eneo la tukio kwenye chumba alimofia Kanumba, ripoti ya uchunguzi wa kifo na maelezo ya onyo ya Lulu.

No comments:

Post a Comment