KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 20, 2013

BAFANA BAFANA ULIMI NJE KWA CAPE VERDE

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

WENYEJI Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana juzi walianza vibaya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Cape Verde.

Katika mechi hiyo ya kundi A, Bafana Bafana ilipata nafasi chache nzuri za kufunga mabao, lakini ilishindwa kuzitumia vyema.

Sare hiyo ilikuwa na faida kubwa kwa Cape Verde, ambayo ni mara yake ya kwanza kucheza fainali hizo, lakini ilionyesha soka ya kuvutia.

Cape Verde ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao katika kipindi cha pili wakati mshambuliaji wake, Platini alipopewa pasi akiwa ndani ya 18, lakini shuti lake lilitoka nje.

Kocha Gordon Igesund wa Afrika Kusini, ambaye alikifanya kikosi chake cha kwanza kuwa siri, aliwashangaza mashabiki wengi wa nchi hiyo baada ya kumwanzisha Lehlohonolo Majoro katika safu ya ushambuliaji badala ya mchezaji mwenye uzoefu, Katlego Mphela.

Bafana Bafana haijawahi kushinda mechi za fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika tangu mwaka 2004. Timu hiyo haikushinda mechi hata moja katika fainali za 2006 na 2008 na ilishindwa kufuzu kucheza fainali za 2010 na 2012.

Kiungo Siphiwe Tshabalala angeweza kuifungia bao Bafana Bafana dakika za mwanzo za pambano hilo kwa mpira wa adhabu, lakini shuti lake lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa Vozhina wa Cape Verde.

Viungo Thuso Phala na Tshabalala walijitahidi kushirikiana vyema na washambuliaji Bernard Parker na Majoro, lakini tatizo kubwa lilikuwa umaliziaji mbovu.

Washambuliaji Heldon Ramos na Ryan Mendes wa Cape Verde walikuwa tishio katika safu ya ulinzi ya Bafana Bafana, lakini hawakuwa makini katika kuipenya.

Mabeki wa kati wa Cape Verde, Fernando Varela na Nando nao walikuwa makini kukabiliana na washambuliaji wa Bafana Bafana na hivyo kuufanya mpira uchezwe zaidi eneo la kati.

Phala alipata nafasi nzuri ya kuifungia bao Bafana Bafana kipindi cha pili baada ye kutengenezewa pasi na Tshabalala, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya goli.

Mara baada ya pambano hilo kumalizika, wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi la Cape Verde walionekana kuwa na furaha kubwa kwa kupata pointi ya kwanza katika fainali hizo, wakati wachezaji wa Afrika Kusini walikuwa na majonzi makubwa.

Kocha Mkuu wa Bafana Bafana, Igesund alisema hakufurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na vijana wake na kuongeza kuwa, kutokana na mchezo waliouonyesha, walistahili kupata sare.

Kocha Mkuu wa Cape Verde,Luico Antunes alisema amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na timu yake na kuongeza kuwa, sare hiyo itawafanya watu 500,000 wa nchi hiyo wawe na furaha.

No comments:

Post a Comment