KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, January 4, 2013

SIMBA, TUSKER HAKUNA MBABE


TIMU ya soka ya Simba jana ilitoka sare ya bao 1-1 na Tusker ya Kenya katika mechi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kuanzia saa moja usiku, Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 18 kupitia kwa Haruna Moshi 'Boban' aliyeunganisha wavuni krosi kutoka kwa Ramadhani Chombo 'Redondo'.

Tusker ilisawazisha dakika ya 39 kwa bao lililofungwa na Khalid Aucho na kuzifanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Licha ya kila timu kufanya mabadiliko kipindi cha pili na pia kushambuliana kwa zamu, hakuna iliyoweza kuongeza bao na hivyo kuzifanya zigawane pointi moja kila moja.

Kwa matokeo hayo, Tusker inaongoza kundi hilo kwa uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, kufuatia kila moja kuwa na pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili.

Hii ni mara ya pili kwa Simba kukutana na Tusker katika muda wa wiki moja. Katika mechi ya kirafiki kati ya timu hizo iliyochezwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilichapwa mabao 3-0 na Tusker.

Katika mechi iliyochezwa jioni, Jamhuri ya Pemba iliichapa Bandari mabao 2-1.

No comments:

Post a Comment