KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 22, 2013

OMOTOLA AANDAA ALBAMU MPYA, KUMSHIRIKISHA AKON

LAGOS, Nigeria

MWITE vyovyote upendavyo, iwe Omotola Jalade, Omo Sex au Omo Milionea, lakini ukweli ni kwamba mwanadada huyo ni sawa na samaki mkubwa ndani ya bahari kubwa.

Katika kudhihirisha ukweli huo, Omotola hivi sasa yupo katika maandalizi ya mwisho ya kurekodi albamu yake mpya ya muziki, kupitia Kampuni na Konvict Music, inayomilikiwa na mwanamuziki nyota wa Nigeria, Akon.

 Omotola ameamua kurekodi albamu hiyo baada ya kuwa kimya kwa kipindi kirefu, akiwa ameelekeza zaidi nguvu zake katika fani ya uigizaji filamu, ambayo imempatia mafanikio makubwa.

Mbali na kucheza filamu, mwanadada huyo, ambaye ni mke wa rubani Matthew Ekeinde na mwenye watoto wanne, pia ameanzisha kipindi maalumu cha televisheni kinachojulikana kwa jina la The Real Omosex.

"Kwa sasa nafanya maandalizi ya kurekodi albamu mpya kupitia kwa watayarishaji muziki Kendrick Dean na Verse Simmonds wa Kampuni ya Konvict Music na tunatarajia kumshirikisha mwanamuziki mmoja maarufu,"alisema Omotola.

Hata hivyo, Omotola hakuwa tayari kutaja jina la mwanamuziki huyo, lakini kuna habari kuwa amepanga kumshirikisha Akon.

Omotola alianza kujuhusisha na muziki mwaka 2006 baada ya kuibuka na albamu yake ya kwanza, inayojulikana kwa jina la Gba kabla ya kuachia albamu ya pili inayokwenda kwa jina la Feel Alright.

Mwanamama huyo alirekodi albamu yake ya pili kwa kushirikiana na mwimbaji na mpiga gita la solo, Harrisong, ambaye pia ni mwalimu wake wa sauti.

Wanamuziki wengine alioshirikiana nao kurekodi albamu hiyo ni prodyuza Del B na mwimbaji Paul PlayDairo. Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo zimepigwa katika miondoko ya Pop na Rock.

"Nyimbo zilizomo kwenye albamu yangu ya pili hazikuweza kupata umaarufu kirahisi. Ni nyimbo zilizolenga kutoa ujumbe. Lengo halikuwa kuvutia watu,"alisema mwanadada huyo mwenye sura na umbo lenye mvuto.

Alipoulizwa ni nani anayemuandikia nyimbo zake, Omotola alisema:" Naziandika mimi mwenyewe, isipokuwa kwa zile, ambazo ninawashirikisha wanamuziki wengine."

Baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Feel Alright ni Get Busy, Harmony, Through the Fire na Barren Land. Kibao cha Barren Land kinaelezea matatizo ya chakula duniani.

Omotola kwa sasa anashika nafasi ya kwanza kwa utajiri miongoni mwa wacheza filamu wa kike nchini Nigeria. Utajiri wake unakadiriwa kufikia Naira milioni 200 za Nigeria.

Mbali na kucheza filamu nyingi, Omotola amerekodi albamu zaidi ya mbili za muziki wa dansi. Kwa kiasi kikubwa, mapato yake yanatokana na filamu, muziki na matangazo ya biashara.

“Ninachokifanya ni kutekeleza majukumu yangu ya siku hadi siku. Ninayatambua na pia nakabiliana nayo kila yanapokuja mbele yangu. Hakuna nisichoweza kukifanya. Kusema kweli nimekuwa na bahati," alisema Omotola.

“Naishi maisha yangu. Naamini kile ninachokiamini. Siishi maisha yangu kwa lengo la kumridhisha mtu yeyote, hivi ndivyo nilivyo.

“Msemo wangu niupendao ni kwamba, kile unachokiona ndicho unachokipata. Kamwe siwezi kusema chochote nyuma yako, ambacho siwezi kukisema mbele yako. Hivi ndivyo nilivyo,”alisema mwanamama huyo mantashau.

No comments:

Post a Comment