KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 15, 2013

'MFUMO WA UTEUZI WA WACHEZAJI TAIFA STARS MBOVU'

KOCHA Mkuu wa zamani wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars na Reli ya Morogoro, Dk. Mshindo Msolla amesema ni vigumu kwa timu inayofundishwa na makocha watatu wa kiwango kinachofanana kuweza kupatikana mafanikio.

Msolla amesema timu inapokuwa na makocha wa aina hiyo na iwapo hawatapeana majukumu, ni rahisi kukaribisha majungu na kuwachanganya wachezaji kwa vile kila mmoja atafundisha kwa mfumo wake.

Kocha huyo mkongwe, ambaye kwa sasa ni mfanyakazi katika Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, alikuwa akijibu swali aliloulizwa kuhusu mtazamo wake baada ya uongozi wa klabu ya Simba kuteua makocha watatu kwa ajili ya kuinoa timu hiyo.

Kwa sasa, Simba inafundishwa na Kocha Patrick Leiwig kutoka Ufaransa, anayesaidiwa na Moses Basena kutoka Kenya na Jamhuri Kihwelu.

Leiwig ameingia mkataba wa kuinoa Simba kwa miezi minane, akichukua nafasi ya Milovan Cirkovic kutoka Serbia, ambaye mkataba wake ulivunjwa baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Basena aliwahi kuwa kocha mkuu wa Simba mwaka jana, lakini mkataba wake ulivunjwa kwa madai ya kutokuwa na vyeti wakati Kihwelu, maarufu kwa jina la Julio, naye amewahi kuifundisha timu hiyo kwa nyakati tofauti akiwa kocha mkuu na kocha msaidizi.

"Mimi naushangaa sana uongozi wa Simba kuwateua makocha watatu, ambao wana sifa zinazoshabihiana. Basena na Julio wameshawahi kuwa makocha wakuu katika klabu tofauti na kupata mafanikio, hivyo sifa zao zinafanana na za Leiwig. Wasipopamgiana majukumu, itakuwa ni kukaribisha majungu,"alisema Msolla.

Akitoa mfano, Msolla alisema kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT), kiliwahi kumteua yeye, marehemu Syllersaid Mziray na Boniface Mkwasa kuwa wasaidizi wa aliyekuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Burkhard Pape kutoka Ujerumani na matokeo yake ni kwamba kulikuwa na mvurugano mkubwa.

Alisema kutokana na kila kocha kuwa na mfumo wake, ilikuwa vigumu kuamua nani aanze kufundisha na wachezaji walikuwa na wakati mgumu wa kuamua wamfuate kocha yupi.

"Ilibidi tulipofika Rwanda kwenye Kombe la Chalenji, tuitishe kikao na kupeana majukumu, "alisema kocha huyo, ambaye kwa sasa ni mtaalamu katika masuala ya kilimo.

Akizungumzia mwenendo wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu, Msolla alisema amefurahishwa na viwango vilivyoonyeshwa na timu za Azam na Coastal Union.

Alisema wachezaji wa Azam wanacheza kwa kujituma na kwa kutumia mfumo unaoeleweka, ndio sababu wamekuwa wakitoa upinzani mkali kwa timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo.

Msolla alisema timu kongwe za Simba na Yanga nazo zinacheza vizuri, lakini kasi yao huwa ni katika dakika za mwanzo na baada ya hapo, wachezaji wanaonekana kuchoka kwa kukosa pumzi na nguvu mwilini.

Hata hivyo, Msolla amezipongeza Simba, Azam na Coastal Union kwa utaratibu ziliouanzisha wa kuwapandisha daraja wachezaji wao wa vikosi vya pili na kuongeza kuwa, iwapo utaratibu huo utakuwa wa kudumu, hazitakuwa na sababu za kusajili wachezaji kutoka nje.

Msolla alisema licha ya kuwepo kwa udhamini wa kampuni kubwa za biashara kwa Taifa Stars, kiwango cha timu hiyo bado kipo chini kutokana na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa na maneno mengi kuliko vitendo.

"Hivi sasa kiwango chetu cha soka kinazidi kushuka chini. Hii ni kwa sababu uteuzi wa wachezaji wa Taifa Stars ni mbovu. Kwa ujumla, wigo na mfumo wa uteuzi wa wachezaji wetu ni mbovu,"alisema kocha huyo.

Akizungumzia ushindi ilioupata Taifa Stars dhidi ya mabingwa wa Afrika, Zambia katika mechi ya kirafiki mwezi uliopita, Msolla alisema ulitokana na bahati zaidi kwa vile timu haikuwa na wachezaji katika safu ya ushambuliaji ya kati.

Alisema ilishangaza kwa mchezaji kama Mrisho Ngasa, ambaye kwa kawaida hucheza kama winga wa pembeni, kuwa mshambuliaji wa kati na kuongeza kuwa, kilichofanyika ni ujanja ujanja kuliko ufundi zaidi.

Msolla alisema Tanzania imejaliwa kuwa na hazina ya wachezaji wengi wenye vipaji vya kucheza soka, lakini tatizo kubwa lipo katika ufuatiliaji wa vipaji, ambao ameuelezea kuwa bado ni mbovu na hautoa nafasi kwa wachezaji wengi, hasa waliopo mikoani kuonekana.

"Viongozi wetu wa soka wanapaswa kuacha ubinafsi na kuweka mbele zaidi maendeleo ya nchi. Vinginevyo, tutaendelea kubaki hapa hapa tulipo sasa,"alisema.

No comments:

Post a Comment