KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 10, 2013

TAIFA STARS KUIVAA ETHIOPIA KESHO

KIKOSI cha timu ya soka ya Taifa, 'Taifa Stars' kinashuka dimbani leo kumenyana na Ethiopia katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa, Ethiopia.

Taifa Stars itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014 dhidi ya Morocco, itakayopigwa Machi 22 mwaka huu.

Kwa upande wa Ethiopia, itautumia mchezo huo kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, zinazotarajiwa kuanza Januari 19 mwaka huu nchini Afrika Kusini.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, maandalizi kwa ajili ya mchezo huo yamekamilika.

Wambura alisema Taifa Stars ilitarajia kufanya mazoezi yake ya mwisho jana jioni katika Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa kwa saa moja kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo na kuongeza kuwa, wachezaji wote wapo katika hali nzuri.

Kwa mujibu wa Wambura, ripoti ya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kim Poulsen imeeleza kuwa, timu ipo katika hali nzuri na inatarajia kufanya vyema katika mchezo huo.

Wambura alimkariri Poulsen akisema kuwa, ushindi kwa timu yake utawafanya wachezaji wajiamini zaidi baada ya mwezi uliopita kuwafunga mabingwa wa Afrika, Zambia bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Taifa Stars itawakosa Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva na Nadir Haroub ‘Canavaro’, ambao wapo na kikosi cha Yanga nchini Ututruki. Pia itamkosa kipa Mwadini Ally, aliyebaki na timu yake ya Azam visiwani Zanzibar na mshambuliaji, John Bocco aliyefanyiwa upasuaji wa goti nchini India.

Wachezaji waliokwenda na Taifa Stars nchini Ethiopia ni makipa Juma Kaseja (Simba), ambaye ndiye nahodha na Aishi Manula (Azam FC). Mabeki ni Aggrey Morris, Issa Rashid, Erasto Nyoni (Azam), Amir Maftah na Shomari Kapombe (Simba).

Viungo ni Salum Abubakar, Khamis Mcha (Azam), Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar) wakati washambuliaji ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- DRC) na Mrisho Ngasa (Simba).

No comments:

Post a Comment