KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 15, 2013

YANGA, BLACK LEOPARDS KUKIPIGA J'PILI

MABINGWA wa soka wa Kombe la Kagame, Yanga wanatarajia kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Black Leopard ya Afrika Kusini, itakayopigwa Januari 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mechi hiyo itakuwa kipimo cha kwanza kwa timu hiyo baada ya kurejea nchini kutoka kambini Uturuki.

Mwalusako alisema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi hiyo, iliyoandaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotions yanakwenda vizuri na wachezaji wana ari kubwa ya kuonyesha makali waliyoyapata walipokuwa Uturuki.

Yanga ilirejea nchini jana alfajiri ikitokea Uturuki ikiwa na kikosi cha wachezaji 27 na viongozi sita na Kocha Ernest Brandts ameamua kuwapa wachezaji mapumziko ya siku mbili.

Kwa mujibu wa Mwalusako, baada ya mapumziko hayo, timu hiyo inatarajia kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo na kufanya mazoezi kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola iliyopo Mabibo, Dar es Salaam.

"Tunashukuru timu imerudi salama na wachezaji wote wapo fiti, isipokuwa wamepewa mapumziko ya siku mbili kabla ya kuendelea na mazoezi kwa ajili ya kujiwinda na mchezo wetu dhidi ya Black Leopord," alisema Mwalusako.

Yanga ilikwenda Uturuki kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara, ikiwa ni pamoja na kucheza mechi tatu za kirafiki za kujipima nguvu.

Katika mechi ya kwanza, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na timu ya daraja la tatu ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani, ilichapwa mabao 2-1 na timu Dinzlispor FC ya Uturuki inayoshiriki ligi daraja la kwanza kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Emmen FC ya Uholanzi.

No comments:

Post a Comment