KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 10, 2013

SAMATTA: NITAIFANYIA MAKUBWA TAIFA STARS

MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta anayecheza soka ya kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, amesema amepanga kuifanyia mambo makubwa timu ya taifa, Taifa Stars.

Samatta alisema hayo mjini Dar es Salaam juzi, muda mfupi kabla ya Taifa Stars kwenda Ethiopia kwa ziara ya mechi moja ya kirafiki.

Mshambuliaji huyo, ambaye amekuwa akishutumiwa kwa kucheza chini ya kiwango anapoichezea Taifa Stars, alisema si kweli kwamba hana uzalendo kwa timu yake ya taifa.

"Habari hizi zinanikera sana. Hivi mimi ningejulikana vipi na TP Mazembe kama sio Taifa Stars na Simba? Wangeniona wapi? Mimi nitaendelea kuichezea timu yangu ya Taifa kwa mapenzi yote ili niwazibe midomo wabaya wangu,"alisema mchezaji huyo.

Alisema yupo tayari kuichezea Taifa Stars wakati wowote atakapoitwa na Kocha Kim Poulsen kwa sababu moja ya sifa za mwanasoka wa kimataifa ni kufanya vizuri katika timu yake ya taifa.

Samatta alisema moja ya ndoto zake ni kuifungia Taifa Stars mabao mengi katika michuano ya kimataifa na pia kuiwezesha kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014 zitakazofanyika nchini Brazil.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu za African Lyon na Simba alisema, kwa sasa yupo fiti baada ya kupona na kusisitiza kuwa, ataanza kuonyesha makali yake leo katika pambano kati ya Taifa Stars na Ethiopia litakalofanyika mjini Addis Ababa.

"Kwa kweli najisikia faraja kubwa leo hii kusafiri na wachezaji wenzangu wa nchi yangu,nina imani mwaka huu nitafanya mengi makubwa, ikiwa ni pamoja na kufunga mabao kwa kushirikiana na wenzangu. Na hilo nitalifanya hata kwa klabu yangu ya TP Mazembe,"alisema nyota huyo.

Samatta alikiri kuwa, kwa sasa anakabiliwa na kibarua kizito cha kupata namba ya kudumu kwenye klabu yake ya TP Mazembe kutokana na kuwepo kwa wachezaji wengi nyota kutoka katika nchi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment