KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, January 7, 2013

TAFF YATOA ONYO KWA WASANII

Na Elizabeth John SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF) limekemea baadhi ya wasanii walioonyesha utovu wa nidhamu katika msiba wa aliyekuwa msanii wa filamu nchini, Juma Kilowoko ‘Sajuki’.

Pia limesisitiza kuwa msanii atakaYeripotiwa katika vyombo vya habari kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu atafungiwa kuigiza.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa TAFF, Simon Mwakifwamba alisema amesikitishwa na kitendo cha wasanii kuacha msiba na kwenda kunywa pombe wakati msiba huo ni wa dini.

Alisema baadhi ya wasanii kuonyesha utovu wa nidhamu katika msiba wa marehemu Kanumba na wengine katika msiba wa Sajuki.

“Nasikitika kuona msanii hajitambui hata kidogo, yaani anaacha msiba anakwenda kunywa pombe tena jirani na mahala pa msiba, jamani huu msiba ni wa dini, hivyo atakayeripotiwa vibaya katika misiba, TAFF tutamfungia” alisema Mwakifwamba.

Katika hatua nyingine, Mwakifwamba alisema msiba huo ulitawaliwa na utani hali ya kwamba umewakutanisha watani wa makabila.

Msiba huo ulitawaliwa na utani baada ya kuwepo kwa wasanii wachekeshaji kama vile, Steven Mengele ‘Steve Nyerere’ ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya fedha, Lucas Mhuvile ‘Joti’ na wengineo wengi.

Wakati huo huo, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imewataka wasanii nchini kujitokeza kushiriki tamasha la sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo litafanyika nchini Rwanda mwezi ujao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kwa Niaba ya Katibu Mkuu, Ofisa Utamaduni Mwandamizi wa Wizara hiyo makao makuu, Habibu Mohamed amesema tamasha hilo lijulikanalo kama JAMAFEST litafanyika kwa siku nane kuanzia Februari 9 hadi 16 mwaka huu.

“ Kwanza napenda kuwajulisha kuwa tumepata mwaliko wa kushiriki Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki, ‘JAMAFEST – 2013’ ambalo ni tamasha muhimu sana kwa wasanii wetu kushiriki katika hatua ya kutangaza na kuuza kazi zao katika soko la sanaa la Afrika Mashairiki,” amesema Habibu.

Amesema kutokana na mwaliko huo wa Jumuiya, Wizara inatoa mwaliko kwa wasanii, asasi, vikundi, wabunifu wa mavazi na kampuni kwa hapa nchini, ambao zitaweza kufanya maonesho na kuuza bidhaa na huduma za Sanaa na Utamaduni, katika mabanda ya Tanzania kutuma maombi yao wizarani ambapo mwisho wa kutuma maombi ni Januari 25. Amesema washiriki watajigharamia nauli ya kwenda na kurudi, chakula na malazi katika kushiriki tamasha hilo.

No comments:

Post a Comment