MABINGWA wa soka wa Kombe la Kagame, Yanga leo wanatarajiwa kushuka dimbani kumenyana na Black Leopards ya Afrika Kusini katika mechi ya kirafiki ya kimataifa, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Yanga tangu iliporejea nchini wiki iliyopita, ikitokea Uturuki, ambako ilikwenda kuweka kambi ya wiki mbili kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Black Leopards, ambayo inashika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi kuu ya Afrika Kusini yenye timu 16, iliwasili nchini jana asubuhi ikiwa na msafara wa wachezaji na viongozi 37.
Mwakilishi wa Kampuni ya Prime Time Promotions, iliyoandaa pambano hilo, Shaffih Dauda alisema jana kuwa, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya pambano hilo yamekamilika.
Dauda alisema wanaamini mechi hiyo itakuwa kipimo kizuri kwa Yanga kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa ligi kuu, inayotarajiwa kutimua vumbi Januari 26 mwaka huu.
Amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo ili kuwapa moyo wachezaji wa kufanya vizuri zaidi. Viingilio katika mechi hiyo ni Sh 30, 000 kwa VIP A, Sh 20, 000 kwa VIP B, Sh 15, 000 kwa VIP C, Sh 7, 000 kwa viti vya rangi ya chungwa na Sh 5, 000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani.
Wakati huo huo, uongozi wa klabu ya Yanga umewataka wanachama wake kuhakikisha kuwa wanalipia kadi zao za uanachama ili waweze kupata haki ya kuhudhuria mkutano mkuu.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mwanachama atakayeshindwa kulipia kadi yake, hataruhusiwa kuhudhuria mkutano huo.
Mkutano mkuu wa Yanga umepangwa kufanyika kesho kwenye bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
Mwalusako alisema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili masuala mbalimbali yanayoihusu klabu hiyo, ikiweko ujenzi wa uwanja mpya na wa kisasa na ule wa jengo la kitega uchumi.
No comments:
Post a Comment