KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, January 28, 2013

BAFANA BAFANA YATINGA ROBO FAINALI




DURBAN, Afrika Kusini

WENYEJI Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana, juzi walifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Morocco.

Sare hiyo iliiwezesha Bafana Bafana kutwaa uongozi wa kundi A ikiwa na pointi tano baada ya kucheza mechi tatu, sawa na Cape Verde, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Morocco, ambayo ilitakiwa kushinda pambano hilo ili isonge mbele, iliweza kuwa mbele kwa mabao mara mbili, lakini mara zote Bafana Bafana ilisawazisha.

Issam El Adoua aliifungia Morocco bao la kuongoza dakika ya 10 baada ya kioa Itumeleleng Khune wa Bafana Bafana kuokoa vibaya mpira wa kona, ukamkuta mfungaji aliyeunganisha wavuni. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

May Mahlangu aliisawazishia Bafana Bafana dakika ya 71 na kuamsha shamra shamra kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.

Mehdi Namli aliiongezea Morocco bao la pili dakika ya 81 kabla ya Siyabonga Sangweni kuisawazishia Bafana Bafana dakika ya 87 na kuufanya uwanja ulipuke kwa mayowe ya kushangilia.

Hii ni mara ya kwanza kwa Bafana Bafana kufuzu kucheza hatua hiyo tangu mwaka 2002 na itabaki mjini Durban kumsubiri mshindi wa pili wa kundi B.

Kutokana na sare hiyo, Morocco imeungana na Angola kufungasha virago kutoka katika kundi hilo, ikiwa ni mara yake ya pili mfululizo kuishia hatua hiyo katika fainali za kombe hilo.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha Gordon Igesund wa Bafana Bafana alisema wanaona fahari kutimiza lengo lao la kwanza la kufuzu kucheza hatua ya mtoano.

"Morocco ilikuwa timu ngumu. Sitaki kutaja makosa, lakini tuliweza kusawazisha mabao mawili. Sasa imesalia michezo miwili kufuzu kucheza fainali na nina imani na wachezaji wangu,"alisema.

Kocha Rachid Taoussi wa Morocco alisema amekatishwa tamaa na matokeo hayo, lakini wachezaji wake walipambana kadri ya uwezo wao.

No comments:

Post a Comment