KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, January 26, 2013

SIMBA, AZAM, COASTAL UNION ZAUA



MABINGWA watetezi Simba leo wameuanza vyema mzunguko wa pili wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika pambano hilo, Simba ingeweza kutoka uwanjani na ushindi mkubwa wa mabao iwapo mshambuliaji wake, Mrisho Ngasa angekuwa makini kila alipolifikia lango la African Lyon.

Ngasa pia alipoteza penalti katika kipindi cha pili baada ya shuti lake kumlenga kipa Abdul Seif. Hadi mapumziko, Simba ilikuwa mbele kwa mabao 3-0.

Mabao ya Simba katika kipindi hicho cha kwanza yalifungwa na Mrisho Ngasa, aliyefunga mawili na Ramadhani Chombo 'Redondo'.

Redondo, aliyerejea Simba akitokea Azam, alifunga bao la kwanza dakika ya tatu baada ya kuunganisha wavuni mpira wa krosi uliopigwa na Ngasa kutoka pembeni ya uwanja na kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki wa Simba.

Bao la pili lilifungwa na Ngasa baada ya gonga safi kati yake na Mwinyi Kazimoto kabla ya kufumua shuti lililompita kipa Seif wa African Lyon.

Lyon ingeweza kupunguza tofauti ya mabao dakika ya 31 wakati ilipopata adhabu ya penalti baada ya beki Paul Ngelema wa Simba kumwangusha Fred Lewis ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, shuti la kwanza la Shamte Ally liliokolewa na kipa Juma Kaseja wa Simba, lakini mwamuzi Israel Mujuni aliamuru penalti hiyo irudiwe. Na iliporudiwa, shuti la Shamte lilitoka pembeni ya lango.

Ngasa aliifungia Simba bao la tatu baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Haruna Chanongo, aliyepandishwa kutoka kikosi cha pili, ambaye alionyesha kila dalili za kuweza kuziba vyema pengo la Emmanuel Okwi, aliyeuzwa kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Lyon ilibadili sura ya mchezo katika kipindi cha pili, ambapo ilicheza gonga safi na kutoa usumbufu mkubwa kwa mabeki na viungo wa Simba, ambao walikuwa wakiutafuta mpira kwa toshi.

Mashambulizi hayo ya Lyon yalizaa matunda dakika ya 59 baada ya kupata bao la kujifariki kupitia kwa Bright Ike baada ya kupokea pasi kutoka kwa Fred.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa leo, Mtibwa Sugar ilichapwa bao 1-0 na ndugu zao wa Polisi kwenye uwanja wa Manungu. Bao pekee na la ushindi la Polisi lilifungwa na Muzamil Saidi.

Katika mechi zingine, Coastal Union iliwacharaza ndugu zao wa Mgambo JKT mabao 3-1, Ruvu Shooting waliwalaza ndugu zao wa JKT Ruvu bao 1-0, Azam iliinyuka Kagera Sugar mabao 3-1 wakati JKT Oljoro iliibamiza Toto Africans mabao 3-1.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo wakati Yanga itakapomenyana na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment