JOHANNESBURG, Afrika Kusini
MABINGWA watetezi, Zambia juzi walianza vibaya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Ethiopia.
Katika mechi hiyo ya kundi C iliyochezwa mjini Nelspruit, Ethiopia ilipata pigo baada ya kipa wake, Jemal Tassew kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkwatua kwa nyuma, Chisamba Lungu.
Kipa huyo alishindwa kuendelea na mchezo na ilibidi atolewe nje ya uwanja kwa machela, lakini alionyeshwa moja kwa moja kadi nyekundu kutokana na kutenda kosa hilo.
Zambia ilikuwa ya kwanza kupata bao muda mfupi kabla ya mapumziko, lililofungwa na Collins Mbesuma baada ya kugongeana vizuri na Isaac Chansa.
Ethiopia ilisawazisha kipindi cha pili kwa bao lililofungwa na Adane Girma kwa shuti la mguu wa kulia lililotinga moja kwa moja wavuni.
Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa Ethiopia katika fainali za Mataifa ya Afrika tangu mwaka 1976. Ethiopia ilishindwa kufunga bao katika fainali za 1982.
Kabla ya bao hilo, Ethiopia ilifanikiwa kupata penalti, baada ya beki, Chisamba Lungu wa Zambia kumwangusha Saladain Said ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, shuti la Said lilipanguliwa na kipa Kennedy Mweene.
Katika pambano hilo, Ethiopia haikuonyesha ugeni wa fainali hizo, licha ya kucheza kwa mara ya kwanza baada ya kuzikosa kwa miaka 31.
Mabeki wa Ethiopia waliwabana vyema washambuliaji wa Zambia huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza na kulifanya pambano hilo liwe na mvuto wa aina yake.
Said alipata nafasi nzuri ya kuifungia bao Ethiopia kipindi cha pili baada ya mabeki wa Zambia kujichanganya, akamtoka beki Joseph Musonda na kubaki ana kwa ana na kipa Kennedy Mweene, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.
Kocha Herve Renard wa Zambia alisema baada ya mchezo huo kuwa, Waethiopia walicheza vizuri na kuongeza kuwa, hakushangazwa na mchezo wao kwa vile alishawatahadharisha wachezaji wake kucheza kwa tahadhari.
"Tunapaswa kumshukuru kipa wetu, bila Kennedy Mweene, tungepata matokeo mabaya,"alisema kocha huyo.
Kocha Sewnet Bishaw wa Ethiopia alisema amefurahi kuona kwamba, licha ya kukosa penalti, wamefanikiwa kupata sare.
Bishaw alisema wachezaji wake wameidhihirishia dunia kwamba wana uwezo wa kucheza soka na alimtetea kipa wake, aliyetolewa kwa kadi nyekundu kwamba alikwenda kuzuia mpira.
No comments:
Post a Comment