KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 15, 2013

JOCELYNE: SIKUTARAJIA KUSHINDA TAJI HILI

JOCELYNE Maro (22) mwezi uliopita aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kushinda taji la mrembo wa Afrika Mashariki baada ya kuwabwaga washiriki wenzake 12 kutoka katika nchi mbalimbali za ukanda huu wa Afrika. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu, mrembo huyo anaelezea ushiriki wake katika shindano hilo na matarajio yake ya baadaye.

SWALI: Wewe ni Mtanzania wa kwanza kushinda taji la mrembo wa Afrika Mashariki tangu mashindano hayo yalipoanzishwa miaka mitano iliyopita. Ulijisikiaje ulipotangazwa kuwa mshindi?

JIBU: Nilifurahi sana. Kwanza nilipatwa na mshtuko kwa sababu sikutegemea kama nitashinda. Sio kwamba nasema mimi mbaya au nini, lakini wenzangu niliokuwa nashindana nao, wote walikuwa wazuri na tulikaa kambini kwa muda mrefu, tulizoeana kwa hiyo nilifurahi sana kwa sababu kushinda shindano hili ni kitu kikubwa sana.

SWALI: Unadhani ni kitu gani kilichokuwezesha kushinda taji hili?

JIBU: Kwa kweli siwezi kujua, majaji ndio wanaojua.

SWALI: Wazazi na ndugu zako waliupokeaje ushindi wako?

JIBU: Walifurahi sana. Mwanzoni Renna Callist (Mratibu wa mashindano haya) aliponiomba na kunishawishi nishiriki kwenye shindano hili, nilikuwa naogopa kumweleza baba na mama. Ni kwa sababu mashindano ya aina hii yamekuwa yakitawaliwa na skendo nyingi. Lakini siku nilipowaeleza, hawakuwa na kinyongo waliniruhusu. Kwa hiyo walifurahi sana baada ya mimi kushinda.

SWALI: Hii ni mara yako ya ngapi kushiriki katika mashindano ya urembo?

JIBU: Ilikuwa mara yangu ya kwanza. Nilikuwa sijawahi kushiriki kwenye mashindano ya aina hii. Hata Renna alipokuwa akinishawishi nishiriki, nilikuwa sijiamini.

SWALI: Kuna dhana iliyojengeka katika jamii kwamba mashindano ya urembo ni ya kihuni. Nini mtazamo wako kuhusu dhana hii?

JIBU: Mashindano ya urembo si ya kihuni. Tatizo lipo kwa baadhi ya washiriki wa mashindano hayo kuyatumia vibaya na hivyo kutoa mwanya kwa vyombo vya habari kuyafanya yaonekane kuwa ya kihuni. Nadhani uhuni ni tabia ya mtu. Lakini wapo wengi walioshiriki kwenye mashindano haya na ambao kwa sasa wamepata nafasi nzuri za kazi katika kampuni mbalimbali.

SWALI: Umejifunza nini kutokana na kushiriki kwenye mashindano haya?

JIBU: Nimejifunza vitu vingi sana kwa sababu wakati tulipokuwa kambini, tulitembelea sehemu nyingi. Tulikwenda Ngorongoro, ambako nilikuwa sijawahi kufika. Nimejifunza vitu vingi kuhusu Tanzania na pia kukutana na washiriki wenzangu kutoka nchi mbalimbali na hivyo kujifunza mengi kutoka kwao, hasa masuala ya kiutamaduni na kimaendeleo. Nilikuwa nafurahia kuzungumza nao kwa sababu ilikuwa nafasi nzuri kwangu kujua mengi kuhusu nchi zao.

SWALI: Nini majukumu yako baada ya kushinda taji la mrembo wa Afrika Mashariki?

JIBU: Moja ya majukumu yangu ni kusaidia kampeni za kupambana na magonjwa ya ukimwi, malaria na kutoa elimu ya magonjwa hayo na mambo mengineyo. Vilevile nitakuwa nikifanyakazi za kuwasaidia wanawake kuwapa moyo na kuinua maisha yao. Inawezekana pia nikaongezewa majukumu mengine, lakini kikubwa kwa sasa ni kutoa elimu ya kupambana na ukimwi na malaria.

SWALI: Kabla ya kushiriki kwenye shindano hili, ulikuwa ukijishughulisha na nini?

JIBU: Nilikuwa chuoni Uingereza. Nilikuwa nachukua shahada ya kwanza katika masuala ya uchumi na biashara. Nilimaliza mwezi Julai ndipo nikaja Tanzania kutafuta kibarua kwa muda ili baadaye nikaendelee na masomo. Lengo langu ni kurudi tena Uingereza kuchukua shahada ya uzamili.

SWALI: Masomo yako ya elimu ya msingi na sekondari ulichukulia wapi?

JIBU: Yote nilisoma Kenya.

SWALI: Kwa maana hiyo hujaishi sana Tanzania?

JIBU: Ni kweli, nilikuwa nakuja na kuondoka, lakini wazazi wangu wote wanaishi hapa Tanzania.

SWALI: Wazazi wako wanajishughulisha na nini kwa sasa?

JIBU: Mama yangu anafanyakazi Agha Khan na baba yangi anafanyakazi TIB (Tanzania Investement Bank).

SWALI: Ni matukio gani ya bahati uliyowahi kukutana nayo katika maisha yako?

JIBU: Kushinda taji la mrembo wa Afrika Mashariki. Ni kitu ambacho sikukitarajia. Kimenifurahisha sana na mpaka hapa nilipo, bado siamini. Ni kama vile bado nipo kwenye mshtuko.

SWALI: Ni tukio gani lililowahi kukuhuzunisha sana katika maisha yako?

JIBU: Kusema ukweli, huwa natokewa na vitu vingi sana, lakini mara nyingi huwa naviacha vipite, sina kawaida ya kuweka kitu rohoni kwangu. Huwa siyapi uzito mambo ya aina hiyi katika maisha yangu. Na yakishapita, nasahau.

SWALI: Unapendelea michezo ya aina gani?

JIBU: Soka na mpira wa kikapu. Nilipokuwa sekondari, nilikuwa nacheza mpira wa kikapu. Nilikuwepo kwenye timu ya shule, lakini nilipokwenda chuo, sijui ikawaje, kazi zilizidi ikabidi niache. Mchezo wa soka napenda kuutazama. Katika ligi ya England, mimi ni shabiki wa Arsenal. Katika ligi ya nyumbani, nafuatilia kidogo lakini sio sana.

SWALI: Unapenda kupika na kula chakula cha aina gani?

JIBU: Napenda sana kula chips na mayai. Pia napenda vyakula vya kiasili kama vile mtori na ndizi. Si unajua sisi wachaga. Pia napenda kula chapati na pilau.

SWALI: Katika siku zijazo, unaweza kufikiria kushiriki kwenye mashindano ya Miss Tanzania? Au unahisi utakuwa umejishusha?

JIBU: Hapana. Sio kwamba nitakuwa nimejishusha, bali hata kushiriki kwenye shindano hili niliamua iwe ni mara moja tu. Kuna vitu vingi ambavyo nimepanga kuvifanya, hivyo sidhani kama nitakuwa na muda tena wa kufanya hivyo.

SWALI: Unapenda kutoa mwito gani kwa wasichana, ambao wangependa kushiriki kwenye mashindano haya, lakini wanaogopa?

JIBU: Napenda kuwaambia kwamba, kushiriki kwenye mashindano haya sio kitu kibaya. Inategemea na mtu mwenyewe alivyo. Kama unajiamini na kujiona unaweza kufanya vizuri, huna sababu ya kuogoa. Kushiriki kwenye mashindano haya kamwe sio uhuni. Wapo warembo wengi walionufaika kutokana na mashindano haya. Huwezi kuonekana mtu tofauti kwa kushiriki kwenye mashindano haya. kama unataka kufanya kitu, fanya.

No comments:

Post a Comment