KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, January 19, 2013

WASAUZI KUZIHUKUMU SIMBA NA LIBOLO

WAAMUZI kutoka Afrika Kusini wamepangwa kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya michuano ya klabu bingwa Afrika kati ya Simba na Clube Recreation Libolo ya Angola.

Pambano hilo limepangwa kufanyika Februari 17 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana wiki mbili baadaye nchini Angola.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mwamuzi wa kati atakuwa Daniel Volgraaff akisaidiwa na Enock Molefe, Lindikhaya Bolo na Lwandile Mfiki. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Emmanuel Lesita kutoka Lesotho.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limewateua waamuzi wanne wa Tanzania kuchezesha mechi ya marudiano ya michuano ya klabu bingwa Afrika kati ya URA ya Uganda na Cotton Sport ya Cameroon.

Wambura alisema jana kuwa, mchezo huo umepangwa kufanyika Machi 3 mwaka huu mjini Kampala, Uganda. Aliwataja waamuzi hao kuwa, Oden Mbaga, atakayekuwa mwamuzi wa kati, akisaidiwa na Jesse Erasmo na Hamis Chang’walu. Mwamuzi wa akiba atakuwa Israel Mujini wakati kamisaa ni Souleiman Waberi wa Djibouti.

Wakati huo huo, CAF imewateua waamuzi wastaafu, Leslie Liunda na Alfred Rwiza kuwa makamishna wa mechi za michuano ya klabu bingwa Afrika.

Wambura alisema Rwiza ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi kati ya APR ya Rwanda na Vital’O ya Burundi itakayochezwa nchini Rwanda kati ya Februari 15 na 17 mwaka huu.

Aliongeza kuwa, Liunda ameteuliwa kuwa kamishna wa mechi ya marudiano kati ya Tusker ya Kenya na St. Michel United ya Seychelles itakayochezwa Kenya kati ya Machi 1 na 3 mwaka huu. Mechi zote ni za raundi ya awali.

No comments:

Post a Comment