'
Thursday, January 24, 2013
LEIWIG-LIGI ITAKUWA NGUMU
KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Leiwig kutoka Ufaransa amekiri kuwa, mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara utakuwa mgumu kwa vile timu nyingi zimefanya maandalizi mazuri.
Leiwig amesema itakuwa vigumu kwake kutabiri timu ipi itakayoibuka na ubingwa na kusisitiza kuwa, timu yoyote itakayocheza vizuri na kushinda ndiyo inayostahili kuwa bingwa.
“Ligi itakuwa ngumu, siwezi kusema kwa sasa iwapo itakuwa rahisi kwa Simba kutetea taji lake,” alisema.
Kocha huyo alisema hayo jana baada ya kikosi cha Simba kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, kikitokea Oman.
Msafara wa timu hiyo uliwasili kwenye uwanja huo saa 11 jioni kwa ndege la Shirika la Oman na kupokewa na baadhi ya viongozi wa timu hiyo, akiwemo Katibu Mkuu, Evodius Mtawala na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu'.
Wachezaji wa timu hiyo walitoka nje ya uwanja kwa mafungu, na kukwepa kupigwa picha na waandishi wa habari. Baadhi ya wakati walitoka nje mmoja mmoja na wakati mwingine wawili wawili.
Leiwig alisema ziara yao ya mazoezi nchini Oman imetoa nafasi nzuri kwake na wachezaji kufahamiana na pia kuwafundisha mfumo anaotumia katika kucheza soka.
Kocha huyo alisema mechi tatu walizocheza dhidi ya timu ya Olimpiki, timu ya Taifa ya Jeshi na Ahli Nasab zilimwezesha kujua uwezo wa kila mchezaji na uimara wa timu yake.
Simba ilikwenda moja kwa moja kwenye hoteli ya Sapphire iliyoko Kigamboni, Dar ee Salaam, ambako itaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania Bara uliopangwa kuanza Jumamosi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment