Na BARAKA KAZIGUTO, ANTALYA
KOCHA Mkuu wa Yanga, Ernest Brandts ametamba kuwa, timu yake kwa sasa iko imara kutokana na wachezaji kuelewa na kufuata vyema mafundisho yake.
Brandts alitoa majigambo hayo juzi licha ya Yanga kuchapwa mabao 2-1 na timu ya Denizlispor FC ya Uturuki katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye viwanja vya Kamelya Complex mjini hapa.
"Timu yangu imecheza vizuri, nadhani wote tulikuwa mashuhuda jinsi vijana wangu walivyoonyesha soka ya kuvutia iliyowashangaza watazamaji,"alisema kocha huyo.
Brandts alikiri kuwa, hakupendezwa na matokeo ya mchezo huo na alimtupia lawama mwamuzi kwa madai kuwa alishindwa kulimudu vyema pambano hilo kutokana na kutoa maamuzi ya kutatanisha.
Mechi hiyo ilikuwa ya pili kwa Yanga tangu ilipowasili Uturuki na kuweka kambi kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Katika mechi yake ya kwanza, Yanga ilitoka sare ya bao 1-1 na timu ya daraja la nne ya Arminia Bielefeld ya Ujerumani.
Katika mechi ya juzi, Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake, Jerry Tegete aliyemalizia gonga safi kati ya Haruna Niyonzima na Athumani Iddi 'Chuji'.
Denizlispor ilisawazisha dakika ya 78 kabla ya kuongeza bao la pili dakika ya 88 kwa njia ya penalti baada ya beki Nadir Haroub 'Cannavaro' kumchezea rafu mshambuliaji mmoja wa timu hiyo.
Yanga iliwakilishwa na Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul, Kabange Twite, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani/Mbuyu Twite, Athumani Idd 'Chuji, Saimon Msuva/Oscar Joshua, Nurdin Bakari, Said Bahanuzi/Didier Kavumbagu,Jerson Tegete/Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima.
No comments:
Post a Comment