'
Sunday, January 27, 2013
ADEBAYOR AIBEBA TOGO
RUSTENBURG, Afrika Kusini
MSHAMBULIAJI Emmanuel Adebayor juzi aliifungia Togo bao moja kati ya mawili, ilipoichapa Algeria mabao 2-0 katika mechi ya kundi D ya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika iliyochezwa mjini hapa.
Matokeo hayo yamefufua matumaini ya Togo kufuzu kucheza robo fainali baada ya kuwa na pointi tatu katika mechi mbili ilizocheza, sawa na Tunisia. Algeria inashika mkia katika kundi hilo.
Togo sasa itacheza mechi yake ya mwisho Januari 31 kwa kupambana na Tunisia na timu yoyote itakayoshinda, itafuzu kucheza robo fainali.
Adebayor aliifungia Togo bao la kuongoza dakika ya 32 kwa shuti la mguu wa kulia lililotinga moja kwa moja wavuni.
Dove Wome aliiongezea Togo bao la pili dakika za majeruhi baada ya kupokea pasi kutoka pembeni ya uwanja, akaingia na mpira ndani ya 18 kabla ya kufumua shuti lililotinga wavuni..
Mechi hiyo ililazimika kusimama kwa dakika 15 ilipotimia dakika ya 86 baada ya mwamba wa goli kupata mushkeli. Maofisa 10 walilazimika kuingia ndani ya uwanja kusimamia utegenezaji wa goli hilo.
"Ilikuwa moja ya mechi ngumu tulizocheza hadi sasa, tulipambana na timu nzuri ya Algeria,"alisema Kocha Didier Six wa Togo.
"Tulikuwa tumedhamiria kushinda na tulistahili kupata ushindi,"aliongeza kocha huyo.
Naye Adebayor alisema amefurahishwa na ushindi huo na kuongeza kuwa, ilikuwa lazima washinde ili kufufua matumaini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment