'
Thursday, January 24, 2013
JK ATETA NA BLATTER
NA MWANDISHI MAALUM, ZURICH
RAIS Jakaya Kikwete amelishukuru Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kwa kuipatia Tanzania misaada mbalimbali ya kifedha na ufundi.
Kikwete amesema misaada hiyo si tu kwamba imekuwa ikisaidia kuinua kiwango cha soka nchini, bali pia barani Afrika.
Rais Kikwete alitoa shukurani hizo jana baada ya kutembelea makao makuu ya FIFA mjini hapa na kukutana na Rais wa shirikisho hilo, Sepp Blatter.
Kikwete aliwasili Zurich akitokea Ufaransa, ambako alifanya ziara ya kiserikali ya siku tatu.
Rais Kikwete ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu, ambapo anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa dunia kuhusu uchumi, utakaofanyika katika mji wa Davos.
Tanzania ni mwanachama wa FIFA kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
FIFA imekuwa ikitoa dola 250,000 za Marekani kila mwaka kwa nchi wanachama kwa ajili ya kuendeleza soka na dola zingine milioni 2.5 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Shirikisho hilo pia limekuwa likitoa dola 400,000 kila baada ya miaka minne kwa kila mwanachama kwa ajili ya malengo ya muda mrefu ya kuendeleza soka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment