'
Friday, January 25, 2013
ZFA YAMKATALIA MAKUNGU KUJIUZULU
Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kimeikataa barua ya maombi ya kujiuzulu iliyowasilishwa na Rais wa chama hicho, Amani Makungu.
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya ZFA kilichofanyika juzi mjini hapa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa, wajumbe wa kamati ya utendaji ya ZFA wamemkatalia Makungu kujiuzulu kwa vile sababu alizozitoa hazijitoshelezi.
Katika barua yake ya kutaka kujiuzulu, Makungu amedai kuwa, amefikia uamuzi huo kutokana na kushindwa kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa chama hicho wa kanda ya Unguja.
Rais huyo wa ZFA amedai kuwa, alipokuwa ziarani Pemba hivi karibuni, hakupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa makamu wake wa Pemba, badala yake alipokewa na viongozi wa chama cha wilaya ya Chakechake.
Aliitaja sababu nyingine iliyomfanya afikie uamuzi wa kujiuzulu kuwa ni viongozi wa ZFA kanda ya Unguja kufanya mambo yao bila kuushirikisha uongozi wa kitaifa na wakati mwingine kuanzisha ligi ya kanda hiyo wanavyotaka wao.
Hata hivyo, wakati wa kikao hicho, wajumbe waliamua kuwa, uamuzi wa Makungu kujiuzulu si sahihi kwa sababu badala ya kutatua matatizo ameamua kuyakimbia.
Katika kikao hicho, wajumbe pia waliona kuwa, Makungu amefanya mambo mengi mazuri tangu alipoingia madarakani ZFA na hivyo yanapaswa kuendelezwa.
Wajumbe waliitaja sababu nyingine ya kupinga uamuzi huo wa Makungu kuwa, usimamizi wa timu ya Zanzibar kwa michuano ya kimataifa kwa sasa umekuwa mzuri na wa kiwango cha juu tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
"Katika mazingira haya, wajumbe wameona kuwa si busara kwa Makungu kuamua kujiuzulu wakati huu, badala yake ashirikiane na wajumbe wenzake kuyatatua matatizo hayo na baada ya hapo ndipo anaweza kujiuzulu," alisema mjumbe mmoja aliyehudhuria kikao hicho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment