'
Sunday, January 27, 2013
IVORY COAST YATINGA ROBO FAINALI KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA
RUSTENBURG, Afrika Kusini
IVORY Coast juzi ilifuzu kucheza robo fainali ya michuano ya soka ya fainali za Mataifa ya Afrika baada ya kuicharaza Tunisia mabao 3-0 katika mechi ya kundi D iliyochezwa mjini hapa.
Ushindi huo umeiwezesha Ivory Coast kuwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, ikifuatiwa na Tunisia na Togo zenye pointi tatu kila moja. Algeria inashika mkia kwa kutoambulia pointi.
Ivory Coast itahitimisha mechi zake Januari 30 kwa kumenyana na Algeria wakati Togo itakipiga na Tunisia.
Iliwachukua Ivory Coast dakika 21 kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Gervinho baada ya gonga safi kati yake na Lacina. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Bao la pili la Ivory Coast lilifungwa na Yaya Toure dakika ya 87 kwa shuti kali la mbali lililotinga moja kwa moja wavuni.
Didier Ya Konan, aliyeingia kipindi cha pili, aliihakikishia ushindi Ivory Coast dakika ya 90 baada ya kuifungia bao la tatu.
Mshambuliaji Didier Drogba, ambaye alionyesha kiwango duni katika mechi ya ufunguzi, aliingia uwanjani dakika ya 67, lakini alishindwa kuonyesha cheche zake.
Katika mechi hiyo, Ivory Coast ilitawala sehemu kubwa ya mchezo na kuonyesha kiwango tofauti na ilivyocheza na Togo.
Tunisia ilifanya shambulizi kubwa dakika ya 84 wakati Saber Khalifa alipoingia na mpira ndani ya eneo la hatari, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Boubacar Barry wa Ivory Coast.
Ivory Coast haijawahi kutwaa kombe la Mataifa ya Afrika tangu 1992. Mwaka jana ilishika nafasi ya pili baada ya kufungwa na Zambia kwa penalti katika mechi ya fainali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment