MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema inazidai klabu za Simba na Yanga jumla ya sh. milioni 253.7 kutokana na kukwepa kulipa kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE).
Kiasi hicho cha fedha ni makato ya PAYE kwa ajili ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa na klabu hizo mbili kwa nyakati tofauti, na ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakatwi kodi kulingana na sheria za kodi nchini.
Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Hamis Lupenja alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mamlaka hiyo inaidai Yanga sh. milioni 203 na tayari imekwishafunga akaunti yake ya benki ya CRDB.
Lupenja alisema Simba inadaiwa sh. milioni 50.7, lakini akaunti ya klabu hiyo bado haijafungwa na wametoa muda kwa viongozi wake kulipa deni hilo kabla ya hatua ya kufungiwa kuchukuliwa.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema TRA imekuwa ikizikumbusha mara kwa mara klabu hizo kongwe nchini kuhusu umuhimu wa kulipa kodi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu.
Alisema hatua ya kuzifungia klabu inakuja baada ya klabu kushindwa kutekeleza wajibu wake na kuongeza kuwa, iwapo klabu hizo zitashindwa kulipa fedha hizo, hatua itakayofuata ni kukamata mali za klabu.
Lupenja alisema zoezi hilo halitaishia kwa klabu za Simba na Yanga, badala yake litafanyika kwa zote, ambazo zimewahi kusajili wachezaji wa kigeni.
"Unajua kwa muda mrefu klabu zetu zimekuwa zikileta wachezaji wa kigeni, lakini hawakatwi kodi na deni linakuwa kubwa, hivyo kwa sasa tumeamua kufuatilia kwa kina na tulianza na baba yao Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na sasa watoto ambao ni klabu," alisema Lupenja.
Alisema lengo la TRA siyo kudidimiza michezo, bali ni kutekeleza wajibu wa kukumbusha watu wote umuhimu wa kulipa kodi.
Mwishoni mwa mwaka jana, TRA ilifunga akaunti ya TFF baada ya shirikisho hilo kudaiwa sh. milioni 157,407.968 zilizotokana na malimbikizo ya PAYE za makocha wa kigeni wa timu za Taifa.
Hata hivyo, akaunti hiyo ilifunguliwa baada ya mazungumzo kati ya TRA, TFF na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa vile fedha hizo zimetolewa na wadhamini, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom kwa ajili ya klabu za ligi kuu.
Alipoulizwa kuhusu hatua, ambazo Yanga imechukua baada ya akaunti yao kufungwa, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrence Mwalusako alikiri kuwa ni kweli akaunti hiyo imefungwa na wameathirika.
Mwalusako alisema akaunti hiyo ndiyo inayopokea fedha za malipo ya kadi za wanachama kabla ya kushiriki katika mkutano mkuu wa klabu hiyo utakaofanyika Januari 19 mwaka huu.
Hata hivyo, Mwalusako alisema uongozi wa klabu yake unaendelea kulishughulikia suala hilo na huenda likatatuliwa hivi karibuni. Hakuwa tayari kutaja hatua wanazotarajia kuchukua.
Viongozi wa Simba hawakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo kwa vile kila walipopigiwa simu, hawakuwa tayari kuzipikea.
No comments:
Post a Comment