KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 24, 2013

TBL YAMWAGA VIFAA VYA MICHEZO KWA SIMBA NA YANGA



KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) imezipatia klabu za Simba na Yanga vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 70.

Vifaa hivyo vyenye nembo ya bia ya Kilimanjaro, ni kwa ajili ya mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika mjini Dar es Salaam jana kuwa, kila klabu imepata vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 35.

Kavishe alisema kampuni yake imekuwa ikizipatia klabu hizo vifaa vipya vya michezo kila zinapokabiliwa na michuano mbalimbali na kwamba wanafurahi kuona zinautumia vizuri udhamini wao.

Alivitaja vifaa vilivyotolewa kwa klabu hizo kuwa ni mipira, viatu vya mazoezi na vya kuchezea mechi, vikinga ugoko, jezi za mazoezi na za kuchezea mechi.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo unatarajiwa kuanza kesho katika viwanja saba tofauti, ambapo Simba itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na African Lyon.

Yanga itaanza mzunguko huo keshokutwa kwa kucheza na Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akipokea vifaa hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema, wanaishukuru TBL kwa kuendelea kuifadhili timu yao.

Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga aliishukuru kampuni hiyo na kusema kuwa, ufadhili huo unasaidia kuifanya timu yao kushiriki vyema katika ligi hiyo.

No comments:

Post a Comment