KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Saturday, January 19, 2013

BAFANA BAFANA KUKATA UTEPE NA CAPE VERDE FAINALI ZA AFRIKA LEO

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

WENYEJI Afrika Kusini, maarufu kwa jina la Bafana Bafana, leo wanafungua dimbani la michuano ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kumenyana na Cape Verde.

Pambano hilo la kundi A linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka barani Afrika, limepangwa kuanza saa 10 jioni (saa 11 kwa Tanzania) kwenye Uwanja wa City wa mjini hapa.

Afrika Kusini ilipewa uenyeji wa fainali hizo mwaka huu baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kuiengua Libya kutokana na kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo mwaka 2011.

Fainali za mwaka huu zitachezwa kwenye viwanja vitano vilivyopo kwenye miji ya Port Elizabeth, Johannesburg, Nelspruit, Durban na Rustenburg, ambavyo pia vilitumika kwa fainali za Kombe la Dunia 2010.

Katika mechi nyingine ya kundi hilo itakayochezwa leo, Angola itamenyana na Morocco kuanzia saa moja usiku kwa saa za Afrika Kusini (saa mbili kwa saa za Tanzania).

Akizungumzia pambano hilo juzi, Kocha Mkuu wa Bafana Bafana, Gordon Igesund alisema wamejiandaa vyema kukabiliana na wapinzani wao na wana uhakika mkubwa wa ushindi.

Igesund alisema baada ya maandalizi ya muda mrefu, anaamini vijana wake watawazodoa wale, ambao wamekuwa wakiiponda timu hiyo kutokana na matokeo ya mechi mbili za kirafiki walizocheza.

Bafana Bafana ilicheza mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Norway na Algeria. Katika mechi ya kwanza, ilichapwa bao 1-0 na Norway kabla ya kulazimishwa kutoka suluhu na Algeria.

"Kama tutakuwa na bahati na kama tutaanza kufunga mabao, nafikiri tunaweza kufika mbali," Igesund aliwaambia waandishi wa habari.

"Natumaini mambo yatakwenda vizuri kwetu kwa sababu tunalo jukumu kubwa na tutakuwa tukiungwa mkono na mashabiki wapatao 90,000 nyuma yetu uwanjani,"alisema kocha huyo.

Hata hivyo, Igesund alikiri kwamba kazi iliyo mbele yao ni ngumu na wanapaswa kuziheshimu timu walizopangwa nazo kundi moja kwa sababu zipo baadhi ya timu, ambazo ni nzuri.

Cape Verde ilifuzu kucheza fainali za mwaka huu kwa matokeo yaliyowashangaza mashabiki wengi wa soka barani Afrika baada ya kuibanjua Cameroon mabao 4-0.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Lucio Antunes alisema juzi kuwa, kikosi chake kina uwezo wa kuvuka hatua ya makundi iwapo wachezaji wake watacheza kwa kufuata maelekezo yake.

Lucio alisema japokuwa ni mara yao ya kwanza kufuzu kucheza fainali hizo, vijana wake wana ari kubwa ya kuonyesha maajabu kwa kushinda mechi ya ufunguzi.

Alisema kama waliweza kuishinda Cameroon katika mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za mwaka huu, haoni kwa nini washindwe kufanya hivyo kwa Bafana Bafana.

Pambano kati ya Angola na Morocco nalo linatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na timu zote mbili kuundwa na wachezaji mahiri, baadhi wakiwa wanacheza soka barani Ulaya.

No comments:

Post a Comment