KLABU ya Simba imemuuza mshambuliaji wake Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia kwa kitita cha dola 300,000 (sawa na sh. milioni 480 za Tanzania).
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' alisema kwa njia ya simu jana kutoka Oman kuwa, Okwi ametia saini mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.
Kwa mujibu wa Kaburu, Okwi alitia saini mkataba huo jana jioni baada ya kufanya mazungumzo binafsi na viongozi wa klabu hiyo.
Kaburu alisema Etoile Du Sahel imeshakamilisha taratibu zote za kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uganda, ikiwa ni pamoja na kumalizana na Simba.
Makamu Mwenyekiti huyo wa Simba alisema, viongozi wa klabu hiyo ya Tunisia wameamua kumsajili Okwi baada ya kuvutiwa na kiwango chake katika mechi mbalimbali walizomshuhudia akiicheza Simba.
Alisema hafla ya utiaji saini mkataba huo kati ya Okwi na viongozi wa Etoile Du Sahel, ilishuhudiwa na Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage.
Kaburu alisema Etoile Du Sahel iliwasilisha maombi ya kumsajili Okwi kwa klabu ya Simba mapema mwezi huu kabla ya kumruhusu kwenda kufanya majaribio.
Okwi alijiunga na Simba miaka minne iliyopita akitokea SC Villa ya Uganda na kuiwezesha kufanya vizuri katika michuano ya ligi na ya kimataifa.
Mwishoni mwa mwaka jana, Simba iliamua kumuongezea mkataba wa miaka miwili mshambuliaji huyo baada ya kuwepo na taarifa kwamba, alikuwa akiwaniwa na klabu za Yanga na Azam.
Okwi alitia saini mkataba huo wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji, iliyofanyika nchini Uganda, lakini haikuweza kufahamika kitita cha pesa alicholipwa, zaidi ya kuongezewa mshahara kutoka sh. milioni 1.5 hadi sh. milioni tatu kwa mwezi.
No comments:
Post a Comment