KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 10, 2013

SIMKOKO ATIMULIWA POLISI MORO

NA DEUSDEDIT UNDOLE

UONGOZI wa timu ya soka ya Polisi ya Morogoro umeamua kuvunja mkataba kati yake na Kocha John Simkoko.

Ofisa Habari wa Polisi Morogoro, Clement Bazo alisema kwa njia ya simu jana kutoka Morogoro kuwa, nafasi ya Simkoko sasa imechukuliwa na Kocha Mohammed Rishard Adolph.

Bazo alisema wameamua kuvunja mkataba na Simkoko kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mechi za mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Alisema wanaamini ujio wa Adolph, atakayekuwa akisaidiwa na Boniface Njohole, utakiimarisha zaidi kikosi hicho kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi hiyo, unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.

Kwa mujibu wa Bazo, Adolph ambaye alikuwa kocha msaidizi wa timu za taifa za vijana na timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, imeingia mkataba wa kuifundisha Polisi Morogoro kwa miezi sita.

Polisi Morogoro ilimaliza mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ikiwa ya mwisho baada ya kuambulia pointi nne katika mechi 13. Ilipata pointi hizo kutokana na kutoka sare katika mechi nne.

Bazo alisema pia kuwa, katika kujiimarisha zaidi, timu hiyo imeamua kumsajili kwa mkopo mshambuliaji Salum Machaku kutoka Simba.

Pamoja na kukatisha mkataba wa Simkoko, Bazo alisema wamepanga kumpa kocha huyo kazi ya kuwa mshauri wa masuala ya kiufundi.

Wakati huo huo, Bazo amesema Polisi Morogoro inatarajia kucheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting kwa ajili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu.

No comments:

Post a Comment