KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 24, 2013

SIMBA, YANGA DIMBANI MEI 18



WATANI wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga wanatarajiwa kurudiana Mei 18 mwaka huu katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano hilo la watani ni miongoni mwa mechi saba za mwisho za ligi hiyo zitakazochezwa siku hiyo kwenye viwanja tofauti, likiwepo pambano kati ya Azam na JKT Oljoro zitakazomenyana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Simba na Yanga zilipambana kwa mara ya kwanza Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Ratiba ya mechi za mzunguko wa pili wa ligi hiyo, iliyotolewa juzi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inaonyesha kuwa, katika mechi zingine za kufunga pazia, Toto African itamenyana na Ruvu Shooting mjini Mwanza, Mgambo JKT itavaana na African Lyon mjini Tanga, JKT Ruvu itamenyana na Mtibwa kwenye uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Prisons itavaana na Kagera Sugar mjini Mbeya wakati Polisi Morogoro watakuwa wenyeji wa Coastal Union mjini Morogoro.

Kwa mujibu wa ratiba, mzunguko wa pili wa ligi hiyo unatarajiwa kuanza Jumamosi kwa mechi sita. Katika moja ya mechi hizo, Simba itamenyana na African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi zingine zitakazochezwa siku hiyo, Mtibwa Sugar itamenyana na ndugu zao wa Polisi Moro kwenye uwanja wa Manungu uliopo Turiani, Morogoro, Coastal Union itawakaribisha ndugu zao wa Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwa, Tanga, Ruvu Shooting itapambana na ndugu zao wa JKT Ruvu kwenye uwanja wa Mabatini uliopo Ruvu mkoani Pwani, Azam itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam wakati JKT Oljoro itacheza na Toto Africans kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Ratiba inaonyesha kuwa, Yanga itaanza mzunguko wa pili wa ligi hiyo Jumapili kwa kumenyana na Prisons kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi zingine zinazotarajiwa kuwa na ushindani mkali ni kati ya Yanga na Mtibwa Sugar zitakazomenyana Februari 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kati ya Yanga na Azam zitakazomenyana Februari 23 kwenye uwanja huo.

Mechi zingine ni kati ya Simba na Mtibwa Sugar zitakazomenyana Februari 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa na kati ya Simba na Azam zitakazomenyana Aprili 13 kwenye uwanja huo.

No comments:

Post a Comment