KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 27, 2013

TEGETE AIPAISHA YANGA





MSHAMBULIAJI Jerry Tegete jana aliwadhihirishia mashabiki wa Yanga kwamba amerejesha makali yake baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matatu ilipomenyana na Prisons ya Mbeya.

Katika pambano hilo la ligi kuu ya Tanzania Bara lililochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliinyuka Prisons mabao 3-1.

Tegete alianza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 10 baada ya kuifungia bao la kwanza, akimalizia krosi maridhawa kutoka kwa Simon Msuva.

Mshambuliaji huyo, aliyeonekana amekwisha wakati wa mechi za mzunguko wa kwanza, aliwainua tena vitini mashabiki wa Yanga dakika ya 66 baada ya kuifungia la tatu. Alifunga bao hilo baada ya kupokea pasi kutoka kwa Nurdin Bakari.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Mbuyu Twite dakika ya 57 baada ya kumalizia pasi ya Didier Kavumbagu, aliyegongeana vyema na Niyonzima. Twite alishangilia bao hilo kwa kubusu logo ya Yanga.

Prisons ilipata bao la kujifariji dakika ya 17, mfungaji akiwa Elias Maguri baada ya kumzidi maarifa Haruna Niyonzima wa Yanga, aliyedhani ameotea.

Maguri nusura aiongezee bao Prisons dakika ya 20 baada ya kupokea pasi kutoka kwa Misango Magai, lakini shuti lake liliokolewa na kipa Ally Mustapha.

Tegete angeweza kufunga bao lingine dakika ya 40 baada ya kutengenezewa pasi safi na Msuva, lakini alichelewa kuupata mpira, kipa David Abdalla wa Prisons alitokea na kuondosha hatari. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.

Kabla ya Tegete kufunga bao la tatu, mlemavu mmoja alitaka kuingia ndani ya uwanja, lakini polisi walimzuia.

Kutokana na ushindi huo, Yanga inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 14, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 27 na Simba yenye pointi 26.

Yanga: Ally Mustapha 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kevin Yondan, Athumani Iddi 'Chuji', Simon Msuva, Nurdin Bakari, Didier Kavumbagu/Hamisi Kiiza, Jerry Tegete, Haruna Niyonzima.
Prisons: David Abdalla, Aziz Sibo, Henry Mwalugala, Lugano Mwangama, Jumanne Elfadhili, Nurdin Issa, Sino Augustino, Fred Chugu, Elias Maguri,Misango Magai na Jeremiah Juma.

No comments:

Post a Comment