MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amechukua fomu ya kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu kwa niaba ya klabu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Manji alichukuliwa fomu hiyo jana na Mwenyekiti wa klabu ya African Lyon, Rahim Kangezi 'Zamunda' kabla ya kuijaza na kuirejesha kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Alipoulizwa sababu za kumchukulia fomu hiyo Manji, Zamunda alisema amefanya hivyo kwa niaba ya klabu za ligi kuu, ambazo ndizo zimempendekeza.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kurejesha fomu hiyo, Manji alisema lengo lake ni kuziwezesha klabu za ligi kuu zijiendeshe kwa kujitegemea.
Manji alisema kwa kuwa klabu kwa sasa zimeundiwa bodi yao, atahakikisha anaisimamia vyema na kujenga misingi imara ya kuzifanya klabu zijitegemee.
Alisema atakuwa tayari kufanya kazi kwa bidii na kuzisaidia klabu ili ziweze kuwa katika hali nzuri kifedha kwa kuzijengea mfumo imara wa kuingiza mapato na kuwa na vyanzo vingine vya fedha.
Uchaguzi mkuu wa viongozi wa Bodi ya Ligi umepangwa kufanyika Februari 22, mwaka huu. Mgombea mwingine aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo hadi sasa ni Said Mohamed, ambaye alichukua fomu Jumatatu iliyopita.
No comments:
Post a Comment