KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, January 20, 2013

MANJI AKUNJUA MAKUCHA YANGA, MWESIGWA, SENDEU WAFUTWA UANACHAMA

MKUTANO Mkuu wa wanachama wa klabu ya Yanga umewavua uanachama aliyekuwa katibu mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa na ofisa habari wa zamani, Louis Sendeu.

Uamuzi wa kuwavua uanachama Mwesigwa na Sendeu ulifikiwa katika mkutano mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jana kwenye bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Mkutano huo ulioongozwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji, ulihudhuriwa na wanachama 1,144.

Mwesigwa na Sendeu walifukuzwa kazi mwaka jana na uongozi wa klabu hiyo kwa tuhuma za utendaji mbovu wa kazi.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Manji alisema wameamua Sendeu na Mwesigwa wafutwe uanachama kutokana na kushindwa kuonyesha uzalendo kwa klabu yao.

Manji alisema licha ya wanachama hao wawili kuidai Yanga, walikwenda kinyume cha katiba kwa kuamua kufungua kesi ya madai mahakamani dhidi ya viongozi wa klabu hiyo.

Mwesigwa alifungua kesi akiidai klabu hiyo sh. 183,400,050 wakati Sendeu anadai sh. 79,900.050.

Manji alisema iwapo wanachama hao wangekuwa na mapenzi na klabu hiyo, wasingeishtaki Yanga mahakamani, badala yake wangekuwa wavumilifu kwa kusubiri malipo yao.

"Hawa ni wanachama wetu, lakini mwanachama aliye na mapenzi na klabu yake hawezi kukimbilia mahakamani kuishtaki," alisema Manji.

Mbali na Mwesigwa na Sendeu, Yanga pia imemfuta uanachama, mwanachama wake aliyetambulika kwa jina moja la Godwion, anayemiliki kampuni ya uwakili ya Auda &Company Advocates kutokana na kuidai klabu hiyo sh. 4,500,000.

Manji alisema, wakili huyo, ambaye alikuwa akisimamia kesi ya madai ya wachezaji Wisdom Ndlovu na Steven Marash, baada ya kumaliza kesi hiyo, aliamua kudai malipo hayo.

"Mwanachama huyu alifanyakazi kimaslahi binafsi na si kwa kutoa mchango kwa klabu yake,"alisema Manji.

No comments:

Post a Comment