KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 15, 2013

SIMBA KULIPA DENI LA TRA KWA MAFUNGU

UONGOZI wa klabu ya Simba umesema utalipa kwa mafungu deni la sh. milioni 50.7 inalodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Deni hilo linatokana na klabu hiyo kukwepa kulipa kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kwa ajili ya wachezaji wake wa kigeni waliosajiliwa na klabu hiyo kwa nyakati tofauti, ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakatwi kodi.

Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari uongozi wa klabu hiyo umeshawasiliana na TRA na kukubaliana kulipa fedha hizo kwa mafungu.

Mtawala alisema wanalikubali deni hilo na kwamba halikwepeki, lakini kutokana na klabu kukabiliwa na majukumu mengi hivi sasa, hawawezi kulilipa kwa mkupuo.

Alisema hiyo ndiyo sababu iliyowafanya wafanye mazungumzo na viongozi wa TRA na kukubaliana kulipa kwa mafungu hadi litakapomalizika.

Alisema lengo la Simba si kukwepa kulipa kodi hiyo. Hata hivyom Mtawala alisema Mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, anatarajia kuzungumzia kwa undani jinsi klabu yake itakavyolipa deni hilo na kulimaliza kabisa.

Wiki iliyopita, TRA kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Walipa Kodi, Hamis Lupenja, ilisema kuwa, TRA inazidai klabu za Simba na Yanga jumla ya sh. milioni 253.7.

Kodi hiyo ni makato ya PAYE ya wachezaji wa kigeni waliosajiliwa na klabu hizo mbili kwa nyakati tofauti na ambao kwa muda mrefu walikuwa hawakatwi kodi kulingana na sheria za kodi nchini.

Lupenja alisema TRA inaidai Yanga sh. milioni 203 na tayari imekwishaifungia akaunti yake ya benki ya CRDB na kwamba akaunti ya Simba haijafungwa kutokana na viongozi wake kupewa muda wa kulipa deni wanalodaiwa.

Alisema hatua ya kuzifungia akaunti za klabu inakuja kutokana na klabu kushindwa kutekeleza wajibu wake na kuongeza kuwa, hatua itakayofuata ni kukamata mali za klabu.

Mwishoni mwa mwaka jana, TRA ilifunga akaunti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kudaiwa sh. milioni 157,407.968 zilizotokana na malimbikizo ya makato ya PAYE ya makocha wa kigeni wa timu za Taifa.

No comments:

Post a Comment