]
YANGA jana iliendeleza ubabe kwa Black Leopards ya Afrika Kusini baada ya kuichapa mabao 2-1 katika mechi ya kirafikiya kimataifa iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ushindi huo ulikuwa wa pili mfululizo kwa Yanga dhidi ya Black Leopards. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 3-2.
Iliwachukua Yanga dakika tatu kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Saidi Bahanuzi, kufuatia shuti la Simon Msuva, aliyepigiwa kona ndogo na David Luhende.
Baada ya kupata bao hilo, Yanga iliongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Leopards, lakini ilipoteza nafasi nzuri za kufunga mabao dakika ya nne, sita na nane.
Leopards ilisawazisha dakika ya 13 kupitia kwa mshambuliaji wake, David Zulu kwa shuti kali lililomshinda kipa Ally Mustapha 'Bathez'. Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1.
Yanga ilikianza kipindi cha pili kwa kasi na kupata nafasi nyingine nzuri za kufunga mabao dakika ya 48, 50 na 52, lakini zilipotezwa na washambuliaji wake kutokana na kukosa umakini.
Katika kipindi hicho, Yanga iliwaingiza Tegete, Athumani Iddi 'Chuji', Haruna Niyonzima, Frank Dumayo na Didier Kavumbagu kuchukua nafasi za Cannavaro, Kabange Twite, Hamisi Kiiza, Bahanuzi na Luhende.
Bao la pili la Yanga lilifungwa na Jerry Tegete kwa njia ya penalti dakika ya 54 baada ya Didier Kavumbagu kuangushwa na beki mmoja wa Leopards ndani ya eneo la hatari. Leopards ilifanya mashambulizi makali kwenye lango la Yanga dakika ya 86 na 87, lakini washambuliaji wake, Mandli Miya na David Zulu walipoteza nafasi hizo za kufunga mabao.
Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twite,Oscar Joshua, Nadir Haroub/Athumani Iddi, Kevin Yondan, Nurdin Bakari/Haruna Niyonzima, Simon Msuva/Nizar Khalfan, Kabange Twite/Frank Dumayo, Hamis Kiiza/Didier Kavumbagu na David Luhende.
Black Leopards: Posnef Omony, Moses Kwena, Thulani Ntshineela, Vicent Mabusela, Victor Kamhuka, Bafana Sibeko, Tuyane Mabunda/Siguve Sibia, Michael Nkambule/ Raymon Monama, Mxolis Gumende, Mandli Miya na David Zulu.
No comments:
Post a Comment