KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, January 15, 2013

TENGA ABWAGA MANYANGA TFF

RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga, ametangaza kutogombea tena wadhifa huo katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Februari 24, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Tenga alisema amefikia uamuzi huo ili kutoa nafasi kwa wadau wengine wa mchezo huo kuliongoza shirikisho hilo.

Tenga alisema muda wa miaka minane alioliongoza shirikisho hilo kwake unatosha na kutokana na umri alionao sasa wa miaka 58, anapaswa kupumzika.

Mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Yanga,Pan African na Taifa Stars alisema, anaondoka madarakani huku akijivunia kujenga misingi imara ya uongozi ndani ya TFF na pia kumaliza migogoroya uongozi iliyokuwa ikitokea mara kwa mara miaka ya nyuma.

Tenga, ambaye aliingia madarakani mwaka 2006 alisema anamshukuru Mungu kwamba katika kipindi chote cha uongozi wake, ameweza kutimiza malengo yake na pia kurejesha amani na nidhamu ndani ya shirikisho hilo.

"Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF wamekuwa wakiniuliza rais vipi, utagombea, lakini nimewaambia mimi hapana kwa sababu mambo yote muhimu nimeshayafanya na kuyatimiza,"alisema.

Alisema chini ya uongozi wake, walifanikiwa kutengeneza katiba nzuri, inayofanana na ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) kama ilivyo kwa klabu zote zinazoshiriki katika michuano ya ligi kuu pamoja na vyama wanachama wa TFF.

Tenga alisema chini ya uongozi wake, waliunda vyombo huru kwa ajili ya kufanya maamuzi, kupanua wigo wa wapiga na kuongeza kuwa, hakuna tatizo lolote linaloweza kutokea kuhusu soka likashindwa kupatiwa ufumbuzi na vyombo husika.

Alisema soka ya Tanzania imekuwa na mvuto kwa mashabiki wakati wa uongozi wake kutokana na kujitokeza kwa kampuni nyingi kuifadhili Taifa Stars na kwamba mashabiki wa soka wamerejesha mapenzi kwa timu hiyo, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Rais huyo wa TFF alisema ameona ni vyema ajiweke pembeni ili kuwapa nafasi wadau wengine wa soka kuendeleza yale yote mazuri aliyoyaanzisha na pia kubuni mambo mapya kwa lengo la kukuza zaidi mchezo huo.

Amewashukuru wadau wa soka nchini na kampuni mbalimbali zilizojitokeza kudhamini mchezo huo kwa kumpa ushirikiano mkubwa wakati wa uongozi wake na kuwataka waendelee kufanya hivyo kwa viongozi wapya.

Tenga amewaomba radhi mashabiki wa soka nchini iwapo aliteleza wakati wa uongozi wake na kuongeza kuwa, ni kawaida kwa kiongozi yoyote baadhi ya wakati kufanya makosa na kisha kujirekebisha.

Ametoa mwito kwa wadau wa soka nchini kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kuwania uongozi wa shirikisho hilo ili waweze kupatikana watu watakaokuwa na mawazo mapya yatakayochochea maendeleo ya mchezo huo.

Alisema atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa kiongozi yeyote atakayechaguliwa kuwa rais mpya wa shirikisho hilo kwa kuwa anaamini bado mchango wake unahitajika katika kuendeleza soka ya Tanzania.

Tenga aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2006 baada ya kuwabwaga mwenyekiti wa zamani wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT), Alhaji Muhidin Ndolanga na Michael Wambura.

Katika uchaguzi huo, nafasi ya makamu wa kwanza wa rais ilichukuliwa na Crescentius Magori wakati nafasi ya makamu wa pili ilichukuliwa na Jamal Bayser.

Tenga alirudi tena madarakani katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2009 baada ya kumbwaga Jamal Malinzi. Katika uchaguzi huo, nafasi ya makamu wa kwanza wa rais ilichukuliwa na Athumani Nyamlani wakati makamu wa pili alikuwa Ramadhani Nassib.

No comments:

Post a Comment