KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, January 24, 2013

MAOMBI YA DHAMANA YA LULU J'TATU



MAOMBI ya dhamana ya msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael 'Lulu', anayesota rumande kutokana na kukabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia, yamepangwa kusikilizwa Jumatatu ijayo.

Lulu anakabiliwa na kosa la kumuua bila kukusudia msanii mwenzake Steven Kanumba.

Taarifa zilizopatika jana katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, zilieleza kuwa, maombi hayo hayataweza kusikilizwa leo kwa sababu ni sikukuu ya Maulid.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maombi hayo sasa yatasikilizwa Jumatatu
mbele ya Jaji Zainabu Mruke.

Lulu kupitia jopo la mawakili, Kennedy Fungamtama, Peter Kibatala na Fulgence Masawe wanaomtetea, aliwasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu kwa kuwa kosa linalomkabili linadhaminika.

Mawakili hao waliwasilisha maombi hayo chini ya hati ya dharura wakiomba yasikilizwe na kuamriwa mapema kwa madai kuwa, Lulu amekaa rumande kwa muda wa miezi saba na kosa lake linadhaminika.

Kwa mujibu wa hati ya maombi iliyoambatanishwa na hati ya kiapo, ambacho muapaji ni wakili Kibatala kwa niaba ya mshtakiwa huyo, wanaiomba Mahakama iamuru mshitakiwa apewe dhamana, akiwa au bila kuwa na wadhamini, au kwa amri na masharti mengineyo ambayo itaona yanafaa.

"Tunaomba Mahakama hii tukufu impe dhamana mshitakiwa akiwa na au bila kuwa na wadhamini, wakati akisubiri usikilizwaji na uamuzi wa kesi yake ya msingi, shauri la jinai namba 125 la 2012, lililopo katika mahakama hii tukufu,” ilisema sehemu ya hati ya maombi.

Lulu anadaiwa kumuua Kanumba bila kukusudia, April 7, 2012, nyumbani kwake (Kanumba), Sinza Vatican, Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, umedai kuwa utaita mashahidi tisa wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo.

No comments:

Post a Comment