MMILIKI wa klabu ya African Lyon, Rahim Kangenzi ‘Zamunda’ (katikati) akirejesha fomu ya kugombea uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu kwa niaba ya Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji (kulia) katika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam jana. Anayepokea fomu hiyo kushoto ni Ofisa wa TFF, Jonathan Aloyce Kakwaya. (Picha kwa hisani ya blogu ya Bin Zubeiry).
Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Yanga, Davis Mosha na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA), Hassan Othman Hassanol, wamechukua fomu za kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mosha alichukuliwa fomu jana na Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa Kilimanjaro, Godluck Moshi wakati Hassanoo alichukuliwa na Ofisa Habari wa COREFA, Masau Bwire.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumchukulia fomu Mosha, Godluck alisema imepita miaka zaidi ya 20 mkoa huo hauna mwakilishi ndani ya TFF hivyo wameona ni vyema wapate mwakilishi.
Godluck alisema Mosha anazo sifa zote za uongozi wa soka na anajua vizuri mambo ya utawala wa michezo hivyo wanaamini akipata nafasi hiyo, atakuwa mwakilishi mzuri wa kanda yao.
Mosha ni mmoja wa wafanyabiashara maarufu katika mkoa wa Dar es Salaam kama ilivyo kwa Hassanoo, ambaye kwa sasa yupo rumande kutokana na kukabiliwa na kesi mbili, moja ikiwa ya uhujumu uchumi.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema jana kuwa, kikatiba, Hassanoo anaruhusiwa kugombea uongozi kama watu wengine kwa vile bado hajapatikana na hatia ya kesi zinazomkabili.
Alisema wagombea wengine 11 walichukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa shirikisho hilo jana na hivyo kufanya idadi ya wagombea kufika 46. Jana ilikuwa siku ya mwisho kwa wagombea kuchukua na kurejesha fomu kwa ajili ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu mjini Dar es Salaam.
Waombaji wapya 11 waliojitokeza jana ni Richard Rukambura, anayeomba urais wakati Kaliro Samson, Jumbe Magati, Richard Rukambura, Omari Walii, Ahmed Mgoyi, John Kiteve, Stanley Lugenge, Francis Ndulane, Riziki Majara na Hassanoo wanawania ujumbe wa kamati ya utendaji.
Orodha kamili ya wagombea ni kama ifuatavyo: Wanaowania urais ni Athuman Nyamlani, Jamal Malinzi, Omari Nkwarulo na Richard Rukambura. Walioomba kuwania nafasi ya makamu wa rais ni Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia.
Wanaowania ujumbe wa kamati ya utendaji ni Salum Chama na Kaliro Samson (Kagera na Geita), Jumbe Magati, Mugisha Galibona, Richard Rukambura, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza), Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo, Elly Mbise na Omari Walii (Arusha na Manyara), Ahmed Mgoyi na Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Blassy Kiondo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama na Stanley Lugenge (Njombe na Ruvuma).
Wengine ni Athuman Kambi, Francis Ndulane na Zafarani Damoder (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi, Geofrey Nyange, Hassan Othman Hassanoo, Riziki Majara na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala, Eliud Mvella na John Kiteve (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir na Shaffih Dauda (Dar es Salaam).
Wakati huo huo, waombaji watatu wapya wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) ambayo uchaguzi wake utafanyika Februari 22 mwaka huu.
Wambura aliwataja waliochukua fomu jana kuwa ni Hamad Yahya wa Kagera Sugar anayeomba uenyekiti wakati Christopher Peter wa Moro United na Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba ya Mwanza wanaoomba ujumbe wa bodi kuwakilisha klabu za Ligi Daraja la Kwanza.
Orodha kamili ya waombaji uongozi wa Bodi ya Ligi Kuu ni Hamad Yahya wa Kagera Sugar na Yusuf Manji wa Yanga wanaoomba uenyekiti wakati Makamu Mwenyekiti aliyeomba ni Said Mohamed wa Azam.
Kwa upande wa wajumbe wawili kuwakilisha klabu za daraja la kwanza ni Christopher Peter Lunkombe wa Moro United ya Dar es Salaam na Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba ya Mwanza.
No comments:
Post a Comment