JOHANNESBURG, Afrika Kusini
IKICHEZA ikiwa na wachezaji 10, Nigeria juzi ililazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Burkina Faso katika mechi ya kundi C ya michuano ya soka ya fainali za Kombe la Mataifa ya iliyochezwa mjini Nelspruit.
Mshambuliaji Alain Traore ndiye aliyeipokonya Nigeria tonge mdomoni baada ya kuifungia Burkina Faso bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi.
Traore alifunga bao hilo baada ya mabeki wa Nigeria kushindwa kuzuia pasi iliyopigwa na Jonathan Pitroipa.
Nigeria ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 23 lililofungwa na Emmanuel Emenike baada ya kupokea pasi kutoka kwa Ideye Brown. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Ikechukwu Uche nusura aiongezee Nigeria bao la pili mwanzoni mwa kipindi cha pili, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.
Nigeria ilipata pigo dakika ya 75 na kulazimika kucheza ikiwa pungufu baada ya beki wake, Efe Ambrose kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Awali beki huyo wa kulia wa klabu ya Celtic ya Scotland alionyeshwa kadi ya njano kipindi cha kwanza kwa kosa la kumchezea rafu Aristide Bance kabla ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu Pitroipa.
Nigeria ililianza pambano hilo kwa kasi na ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 12 wakati Brown alipopewa pasi maridhawa na Ahmed Musa, lakini shuti lake lilipaa juu ya lango.
Wanigeria walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, ambapo Burkina Faso ilishindwa kufanya mashambulizi ya maana.
Nafasi pekee nzuri kwa Burkina Faso kufunga bao katika kipindi hicho, ilipatikana dakika ya 39 wakati nahodha Moumouni Dagano alipojitwisha kwa kichwa krosi ya Pitroipa, lakini mpira ulipaa juu ya lango.
Nigeria, ambayo ilitwaa taji la michuano hiyo kwa mara ya mwisho 1994, inatarajiwa kushuka tena dimbani Ijumaa kumenyana na mabingwa watetezi, Zambia wakati Burkina Faso itamenyana na Ethiopia.
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Stephen Keshi wa Nigeria alisema, anajivunia wachezaji wake kwa kucheza alivyotaka na kusisitiza kuwa, mechi yao dhidi ya Zambia itakuwa na umuhimu mkubwa.
Kocha Paul Put wa Burkina Faso alisema kutokana na timu zote za kundi hilo kuwa na pointi moja, nafasi ipo wazi kwa kila mojawapo kufuzu kucheza hatua ya pili.
Put aliwapongeza vijana wake kwa kuonyesha kiwango kizuri cha soka na kuongeza kuwa, alikuwa na uhakika wa kupata pointi kutoka kwa Nigeria.
No comments:
Post a Comment