'
Tuesday, January 8, 2013
SIMBA YAENDA OMAN KWA MAFUNGU
TIMU ya soka ya Simba inatarajiwa kuondoka nchini leo jioni kwenda Oman kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki mbili ya kujiandaa kwa mzunguko wa pili wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zilieleza jana kuwa, kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuondoka saa 10 jioni kwa ndege ya Shirika la Emirates.
Hata hivyo, habari hizo zimeeleza kuwa, Simba itakwenda Oman kwa mafungu, kufuatia baadhi ya wachezaji wake kuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars na wengine kwenye kikosi kinachoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, kikosi kitakachoondoka leo kitaongozwa na Kocha Msaidizi, Jamhuri Kihwelu.
Hata hivyo, haikuweza kufahamika ni wachezaji wangapi watakaoondoka leo kwa vile uamuzi wa mwisho ulitarajiwa kutolewa jana jioni na Kocha Mkuu, Patrick Liewig.
Wachezaji wa Simba walioko kwenye kikosi cha Taifa Stars, kitakachoondoka leo kwenda Ethiopia ni Juma Kaseja, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Amri Kiemba,
Mwinyi Kazimoto na Mrisho Ngasa.
Wachezaji hao wanatarajiwa kwenda Oman wakitokea Ethiopia, ambako Taifa Stars itacheza na timu ya taifa ya nchi hiyo, katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayopigwa keshokutwa mjini Addis Ababa.
Mmoja wa viongozi wa Simba alisema wachezaji wengine wa timu hiyo walioko Zanzibar, wanatarajiwa kuondoka nchini Jumapili wakiongozana na Kocha Leiwig.
Simba inatarajiwa kushuka dimbani kesho kumenyana na Azam katika mechi ya pili ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Amaan. Kikosi kitakachocheza mechi hiyo kinaundwa na wachezaji wengi waliopandishwa daraja kutoka kikosi cha pili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment